
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli kwa mara ya kwanza amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti
ya chama hicho.
Magufuli pia amekutana na
wafanyakazi wa CCM Makao Makuu katika Ofisi za Chama hicho Mjini Dodoma ikiwa
ni siku tano tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa Tano wa Chama hicho.
Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli amekutana na watendaji hao wa CCM kwa lengo la kuwasalimia, kupokea
maoni na ushauri wao juu ya utendaji kazi ndani ya Chama.
Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti
wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewapongeza watendaji wote
wa Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa namna ya pekee kwa
jinsi walivyotoa mchango mkubwa kuhakikisha CCM inapata ushindi katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana.
Pia amewataka kuendelea kufanya
kazi kwa juhudi na maarifa kwa lengo la kuendelea kukiimarisha Chama hicho
ambacho kimebeba dhamana ya kuongoza Serikali kwa kipindi kingine cha miaka
mitano.
Dkt. Magufuli amewahakikishia kuwa
chini ya uongozi wake atafanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili
watumishi wa CCM ikiwemo maslahi duni, vitendea kazi na kuondoa utegemezi.
Aidha, Dkt. Magufuli amewataka
watumishi wa chama kutoa ushirikiano katika zoezi la uhakiki wa mali za Chama
litakalosimamiwa na sekretarieti ya chama na ameahidi kuwa atahakikisha mapato
yatokanayo na vyanzo vya mapato vya chama yanatumika ipasavyo.
Kwa upande wao watumishi wa CCM
wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ndugu Abdulrahaman Kinana
wamempongeza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwa asilimia mia
moja na wajumbe wa Mkutano Mkuu uliofanyika tarehe 23 Julai, 2016 Mjini Dodoma
kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa.
Watumishi hao wamemuahidi
kuendeleza utumishi uliotukuka na wameelezea matumaini yao ya kuboreshewa
maslahi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na
Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa.

No comments:
Post a Comment