
CHUO Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), kimetoa ufafanuzi wa taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa vyuo vyake vishiriki vimezuiwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kufanya udahili wa wanafunzi.
Taarifa hizo zinazosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii zimedai kuwa vyuo vishiriki vya SAUT ambavyo ni Stella
Maris Mtwara University College (STEMMUCO) na Archbishop James University
College (AJUCO) vimefungiwa na TCU kufanya udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa
masomo 2016/2017.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo
vya habari iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo cha SAUT, Dk Thadeus Mkamwa,
taarifa hizo ni za upotoshaji na kuwa hawajapokea taarifa kutoka TCU ikivizuia
vyuo hivyo viwili kufanya udahili.
Aidha, Dk Mkamwa aliiomba jamii na
wadau wa elimu kwa ujumla kupuuzia taarifa hizo kwa kuwa zina uwezekano wa kuwa
ni mbinu chafu zinazofanywa na baadhi ya watu kuuhadaa umma hasa katika kipindi
hiki ambacho ni muafaka kwa waombaji kufanya maombi katika vyuo vikuu.
“Tunauomba umma
wa Watanzania kufahamu kuwa, Chuo Kikuu cha SAUT na vyuo vyake vikuu vishiriki
vilivyotajwa hapo juu vinaendelea na udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo
2016/2017,” alisema Dk
Mkamwa.
Alisema SAUT ni Chuo Kikuu
kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania, na kwamba kimepiga hatua kubwa
katika kujiendeleza na kufanikiwa kuanzishwa kwa vyuo vingine vikuu vishiriki
vya SAUT ambavyo ni STEMMUCO kilichopo Mtwara, AJUCO kilichopo Songea na Jordan
University College (JUCO) kilichopo Morogoro.
Vyuo vingine ni St. Francis
University College of Health and Allied Sciences (SFUCHAS)- Morogoro,
Archbishop Mihayo University College (AMUCTA)- Tabora, na Cardinal Rugambwa
Memorial University College (CARUMUCO) kilichopo Bukoba, Marian University College
(MARUCO) kilichopo Bagamoyo.
Dk Mkamwa aliongeza kuwa, chuo
kimeweza kuanzisha vituo vingine vitatu vya SAUT vilivyoko Mbeya, Arusha na Dar
es Salaam.

No comments:
Post a Comment