RAIS John Magufuli amemwahidi kwa
utani kumpatia kazi Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, endapo
atafukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kusifia
kazi inayofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza na wageni waalikwa
waliofika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana, kushuhudia
shughuli ya makadhibiano ya madawati ambayo yalitokana na Sh. bilioni nne
ambazo zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ikiwa ni mpango wake wa
kubana matumizi, Rais Magufuli alisema amekuwa akivutiwa na ‘statement’ (kauli)
ambazo zimekuwa zikitolewa na meya huyo.
Alisema hata alipompatia nafasi ya
kuwasalimia wananchi waliofika kwenye hafla hiyo, meya huyo aliongelea masuala
muhimu yenye kuleta maendeleo kwa taifa.
Rais Magufuli alisema amekuwa
akifuatilia kauli za Meya Mwita na kueleza hotuba zake zimekuwa zenye dhamira
ya kuleta maendeleo.
Alisema kwa mzaha, ikiwa meya huyo
atafukuzwa katika chama chake yeye atamkumbuka kwa sababu bado amebakiwa na
nafasi nyingi za uteuzi.
“Ninafurahi Meya Mwita,
ninakupongeza sana kwa sababu nimekuwa nikisikiliza sana `statement’ zako za
maendeleo, sasa sijui nikisema hivi watakubakiza au watakufukuza, ila
wakikufukuza mimi nitakukumbuka kwa sababu nina nafasi nyingi bado za uteuzi,” alisema Rais
Magufuli kwa utani na kusababisha watu kucheka.
Alisema viongozi wanapaswa kulenga
kutatua matatizo ya wananchi na siyo kuingiza masuala ya itikadi za vyama
katika kila jambo.
Awasifu Dr Tulia na Mchungaji
Msigwa
Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli aliwapongeza Mbunge wa Iringa (Chadema), Peter Msigwa na Naibu Spika
wa Bunge, Dk. Ackson Tulia, kwa kukaa pamoja katika meza kuu wakati wa hafla
hiyo.
Wabunge kutoka vyama vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitangaza kususia vikao vya bunge
vinavyoongozwa na Dk. Ackson au shughuli yoyote itakayoongozwa naye kwa madai
amekuwa akiendesha vikao vya bunge kwa upendeleo na kutaka avuliwe wadhifa huo.
Rais Magufuli alisema inapofika
masuala ya kuleta maendeleo ya taifa, viongozi wanapaswa kuweka kando masuala
ya vyama.
Alisema hata yeye wakati akipiga
kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, aliwaahidi Watanzania kuwa atawatumikia
wote bila ya kuangalia vyama, kabila, dini wala rangi.
“Mmeacha vyama vyenu pembeni,
mnaunga mkono maendeleo, leo unapomwona Msigwa na Tulia wapo jirani inatia
moyo, ndicho tunachokitaka, nchi hii ni yetu sote, tukifanya hivyo nchi yetu
itakuwa ya mfano,” alisema Rais Magufuli.
Alipoulizwa kwa kitendo chake cha
kuhudhuria shughuli hiyo na kukaa meza moja na Dk, Ackson, Msigwa alisema
wamefika katika hafla kama wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge.
Alisema pia walihudhuria hafla hiyo
kwa sababu ni suala la maendeleo na walipaswa kushiriki ili kuhakikisha fedha
hizo zinatumika kama zilivyopangwa.
“Hii shughuli haiendeshwi wala
kuandaliwa na Tulia, ni shughuli iliyoendeshwa na tume yetu na ndiyo maana tupo
hapa,” alisema Msigwa.
Pia Rais Magufuli alimtaka Mbunge
wa Kaliua(CUF), Magdalena Sakaya, kutoogopa kupeleka maendeleo katika jimbo
lake kwa sababu maendeleo hayana chama
Mbunge huyo alisema hafla hiyo ni
ya maendeleo hivyo hawakuwa na sababu ya wao kugomea.
Wabunge wa Ukawa waliwahi
kukaririwa wakilalamikia kitendo cha uongozi wa Bunge kurejesha Sh. bilioni nne
serikalini ili kubana matumizi.
Rais Magufuli, ambaye alikabidhiwa
hundi ya fedha hizo Aprili 11, mwaka huu, alielekeza zitumike kutengeneza
madawati, huku akizitaka ofisi na taasisi zingine za serikali kuiga mfano huo.

No comments:
Post a Comment