
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne,
Jakaya Kikwete amesema yuko tayari kuitumikia Afrika kwa nafasi ya Mwenyekiti
wa Kamisheni ya Afrika katika Umoja wa Afrika (AU), ikiwa atapewa majukumu hayo.
Alisema akiteuliwa kushika nafasi
hiyo atakubali, lakini hawezi kuiomba kwa kuandika barua.
Alisema hayo jana Dar es Salaam
alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kutajwa kwa jina lake kwamba ana
nafasi kubwa ya kushinda nafasi hiyo katika uteuzi utakaofanywa siku chache
zijazo ili kumrithi Mwenyekiti wa sasa, Nkosazana-Dlamini Zuma wa Afrika Kusini.
“Inawezekana mtu alikaa mahali
akasema hawa ndio watatu wanaweza kutufaa, lakini mimi siwezi kuandika barua
kuomba kazi yoyote,”alisema.
Mwanadiplomasia huyo maarufu
alisema amefanya kazi kubwa kuliko zote ambazo binadamu anaweza kufanya ambayo
ni kazi ya kuwa Rais wa nchi yake, hivyo hakusudii tena kuandika barua ya
kuomba kazi. Alisema kama viongozi wa Afrika wakiamini kuwa anaweza kushika
nafasi hiyo na kuongoza, yuko tayari kujitolea kama kiongozi wa Afrika, lakini
si kuiomba.
Alisema, “Ili kuwa
Mwenyekiti lazima uombe, mimi si mgombea na waliogombea wapo. Watu wananiombea
heri, In Shaa Allah, lakini haliwezekani kwa sababu sijaomba.”
“Naandika barua na nani anaomba na
mwingine anaomba, hapana jamani si vizuri. Wakiridhika viongozi wa Afrika
wakasema hapa tunakuomba utusaidie ntafanya siwezi kuipa Afrika kisogo,” Kikwete alisema.
Katika tukio jingine, Kikwete
alizitaka nchi za Afrika zinazoingia katika mapinduzi ya viwanda kuzingatia
athari za tabia nchi zenye madhara makubwa.
Alitoa rai hiyo alipokuwa akifungua
mkutano wa siku mbili wa watafiti na wataalamu wa athari za mabadiliko ya tabia
nchi duniani, unaojadili namna ya kutekeleza mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko
ya tabia nchi.
Alisema nchi isipopanga maendeleo
yake vizuri itafika mahali mazingira yataharibika na kuwa na madhara makubwa,
hivyo ni wajibu wa nchi zote duniani kulishughulikia.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, alimtaja Kikwete kuwa shujaa aliye mtari wa
mbele kupambana na tatizo hilo la athari za tabia nchi.

No comments:
Post a Comment