
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwachukulia
hatua watumishi wote wa sekta ya afya wanaojihusisha na wizi wa dawa.
“Fuatilieni na
kuwachukulia hatua watumishi wa Zahanati wanaoiba dawa. Hawa hawana nafasi ya
kuendelea kufanya kazi kwa sababu ni wauaji,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo juzi
jioni (Jumamosi, Agosti 20, 2016) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Katavi
mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Alisema kila kiongozi kwenye eneo
lake ahakikishe dawa zinazopelekwa na Serikali kwa ajili ya kuwahudumia
wananchi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Pia ameitaka Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) kujenga duka la dawa mkoani Katavi kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji
wa dawa katika mkoa huu pamoja na mikoa jirani.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
aliwataka Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari
wasiokuwa na shahada waende wakasome kama wanahitaji kuendelea kuwa na wadhifa
huo.
Alisema Mratibu wa Elimu katika
ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya
kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari na msingi.
Kwa upande wa walimu wakuu katika
shule za msingi, Waziri Mkuu alisema ni lazima wawe na diploma, hivyo aliwataka
walimu wakuu wote wasiokuwa na diploma kwenda kusoma kabla hawajaondolewa
kwenye wadhifa huo.
Alisema Serikali imetenga zaidi ya
sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka, ambapo Waratibu Elimu
Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu
wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja
Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga alisema mkoa umeendelea kuongeza bajeti ya
dawa ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika ngazi zote za kutolea huduma.
“Mwaka 2012
bajeti ya dawa na vifaa tiba ilikuwa sh. Milioni 558 ambayo ilitosheleza
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa asilimia 70. Katika bajeti ya mwaka
2016/2017 mkoa umetengewa jumla ya sh bilioni 1.3 ambayo tunaamini itamaliza
tatizo la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mfumo
mpya wa usambazaji dawa kupitia MSD umesaidia dawa, vifaa tiba na vitendanishi
kupelekwa moja kwa moja hadi katika ngazi ya zahanati hali iliyosaidia dawa
kufika kwenye vituo vya kutolea huduma kwa asilimia 100.
Mapema jana Waziri Mkuu alifanya
ziara katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambapo alisema Serikali
itahakikisha hospitali hiyo inaongezewa huduma zaidi kwa sababu ni ya wilaya
ila inahudumia wagonjwa wa mkoa wote.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI
21, 2016.

No comments:
Post a Comment