
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
kuwa wakimbizi waliopewa uraia wa Tanzania na kuitumia vibaya nafasi hiyo kwa
kuingiza watu wengine kinyume cha sheria watanyang’anywa na kurudishwa
walikotoka.
Aidha, Waziri Mkuu amewaomba
viongozi wa dini wawe wanawaelimisha waumuni wao umuhimu wa kulinda amani na
kuishi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi husika.
Kauli hiyo imetolewa jana (Jumapili,
Agosti 20, 2016) na Waziri Mkuu wakati akizungumza na waliokuwa wakimbizi wa
Burundi ambao kwa sasa wamepewa uraia wa Tanzania wanaoishi katika Kata ya
Katumba, Halmashauri ya Nsimbo wilayani Mpanda.
“Wakimbizi
waliopewa uraia wameendelea kuingiza ndugu zao. Naagiza kamati ya ulinzi na
usalama ya mkoa ifanye ukaguzi katika kambi zote kwa sababu zimegeuzwa kuwa
maficho ya kuwahifadhi watu wanaoingia nchini bila ya vibali,” alisema.
“Hakikisheni
mnachukua hatua kwa wote watakaoingiza watu kinyemela katika kambi za wakimbizi
za Mishamo na Katumba. Pia msiruhusu watu kuleta silaha kwenye maeneo haya.
Tanzania watu wanaoruhusiwa kutembea na silaha ni askari tu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alisema lazima ulinzi
uimarishwe katika maeneo ya mipakani na wasipofanya hivyo watu wengi wataingia
nchini bila ya kuwa na vibali hivyo kusababisha ongezeko kubwa la idadi ya
watu.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda wasiwaudhi wakulima na
wafanyabiashara wadogo kwa kuwatoza ushuru kwenye mazao wanapotoka
shambani kama debe moja la nafaka na wanaouza bidhaa ndogo ndogo.
“Mkulima ametoka
shambani na debe moja la mahindi unamtoza ushuru maana yake nini? Halmashauri
tusitafute mgogoro katika hili. Tafuteni biashara za kutoza ushuru, mkulima
anatoka kijiji cha Kanoge anakwenda kijiji cha Ikongo ushuru wa nini?" Waziri Mkuu
alihoji.
Waziri Mkuu alisema “Tumewasisitiza
mkusanye kodi lakini siyo hivyo. Mkiendelea kutoza ushuru kwa wakulima
wanaotoka shambani na mahindi kidogo mtasababisha wakate tamaa ya
kulima,”.
Akisoma taarifa ya maendeleo ya
mkoa wa Katavi jana jioni (Jumamosi, Agosti 20, 2016) mara baada ya Waziri Mkuu
kuwasili mkoani hapa Mkuu wa mkoa, Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga
alisema mkoa una jumla ya wakimbizi 6,918 wanaoishi katika kambi za Mishamo na
Katumba ambapo kati yake wakimbizi 2,150 waliomba uraia wa Tanzania na
kunyimwa.
Alisema wakimbizi 2,489 walichagua
kurejea nchini kwao Burundi ila bado wapo katika kambi hizo huku wengine 653
waliomba uraia lakini majina yao hayakuonekana kwenye orodha ya waliokubaliwa
wala kukataliwa uraia hivyo mkoa unaendelea kufuatilia ili kujua hatma
yao.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa
wakimbizi wengine sita walichagua kubaki nchini lakini hawakuomba uraia, 398
waliomba uraia ila fomu zao hazikukamilika,249 waliomba uraia ila majina yao
hayakurudi huku wengine 973 hawakusajiliwa walipoingia nchini mwaka 2007/.2008.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 21, 2016.

No comments:
Post a Comment