
MABASI yanayosafirisha abiria
wanaokwenda mikoani yaliyofungiwa na Serikali kwa kusababisha ajali yameanza
kuruhusiwa kutoa huduma hiyo.
Mabasi hayo yameruhusiwa baada ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (SUMATRA) na Wamiliki wa
Mabasi ya Abiria (TABOA) kufikia muafaka.
Makubaliano hayo yaliyofanyika
mwishoni mwa wiki iliyopita yalilenga kuleta suluhu kwa kuwataka TABOA
kusimamisha mgomo wa mabasi uliopangwa kufanyika nchi nzima Agosti 22 mwaka
huu.
Zaidi ya mabasi 60 ya kampuni
tofauti yalifungiwa na Serikali baada ya kile kilichodaiwa na serikali kwamba
yalisababisha ajali kwa uzembe wao.
Wamiliki wa mabasi hayo walikuwa
wanahoji sababu ya SUMATRA kufungiwa leseni ya usafirishaji kwa kampuni
badala ya kupewa adhabu basi moja lililopata ajali badala ya kufungiwa kampuni
nzima.
Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu
jana alisema wamekubaliana mabasi ambayo ni mazima yaliyofungiwa yaachiwe
kutegemeana na utaratibu wa ukaguzi yaweze kuingia barabarani kutoa huduma ya
usafirishaji.
“Tulikubaliana na serikali ndani ya
siku saba iwe imeyafungulia mabasi yetu mazima kutegemeana na utaratibu wa
ukaguzi yaendelee kutoa huduma kwa wananchi na tayari serikali imeanza
kuyaachia baadhi ya mabasi hayo,
“Baadhi ya mabasi yaliyofungiwa
ambayo yameachiwa kutoa huduma ni ya Mohammed Trans, Mbazi, Kisbo Safari,
City Boy, KVC, Wibonera na Kandahari”, alisema Mrutu.
Alisema walikubaliana serikali
iyakamate mabasi yote madogo nchini yanayofanya safari za usafirishaji abiria
mikoani bila ya kuwa na leseni ya biashara hiyo.
Alisema mabasi hayo yamekuwa kero
kubwa kwa kugombania abiria na yanapokuwa barabarani yanawachomekea madereva wa
mabasi makubwa.
Pia aliomba idadi ya vituo vya
polisi vya ukaguzi barabarani vipungue.

No comments:
Post a Comment