OKTOBA Mosi (1) ya kila mwaka ni siku iliyoteuliwa na Umoja wa
Mataifa kuadhimisha uwepo wa wazee katika jamii kote ulimwenguni.
Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi Oktoba 1, 1991 kwa lengo la
kuongeza uelewa kuhusu mambo yanayowalenga wazee ikiwemo kutoheshimu haki za
wazee, kutazama mahitaji na maslahi ya wazee na kuhakikisha mzee popote alipo
ulimwenguni anapata huduma za msingi za kijamii kama vile huduma bora za afya
na matibabu.
Mahususi, siku hii imekuwa na lengo la kuutambua mchango wa
wazee katika jamii kwa wakati husika na wakati uliopita katika mataifa yao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunatumia fursa hii kuwapongeza wazee wote
duniani na hususan wazee wa Tanzania.
Pia tunatumia siku hii kuikumbusha serikali na mihimili
mingine ya dola pamoja na wanachi wote kwa ujumla kuheshimu wazee
wetu kama hazina ya taifa. Pia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitumia
siku hii kuungana pamoja na wazee wanaodai haki yao kwa zaidi ya miaka
20.
Mathalani, wazee waliotumikia iliyokuwa jumuiya ya Afrika
Mashariki kabla ya kuvunjika kwake mwaka, 1977 ambao mpaka leo wameendelea
kupambana na kudai haki yao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pia tunaitumia siku ya leo
kuitaka serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania kutoa msimamo
wake juu ya kesi ya madai ya waliokuwa walinzi wa ubalozi wa marekani nchini
Tanzania wakijulikana kama 'mission security force' katika Ubalozi wa Amerika
kwa serikali ya Amerika – 1984.
Sambamba na hayo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinakemea
vikali vitendo vya mauji ya wazee kwa imani za kishirikina vinavyozidi kupamba
moto nchini, watoa huduma wa afya wanaotumia lugha za kuudhi dhidi ya wazee,
vijana wanaorubuni wazee kuuza mali zao na kuwatapeli hususani ardhi kuacha
vitendo hivi ili kuheshimu tunu hii adhimu ya Taifa..
Tunaungana na jamii ya ulimwengu kusimama kupinga mitazamo hasi
juu ya wazee na uzee kiujumla.
Wazee ni hazina kwa Taifa tuilinde hazina hii kwa uendelvu wa
jamii yetu.Tuwatunze na kuwasikiliza wazee wetu.
Imetolewa jana Tarehe 1/10/2016
Dkt.Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji.
No comments:
Post a Comment