MKURUGENZI wa kiwanda cha magodoro
cha Dodoma Asili Bw. Haidary Gulamali amesema atawaleta madaktari bingwa 14
kuja kufanya upasuaji wa moyo bure kwa watoto watakaobainika kuwa na matatizo
hayo.
Amesema madaktari hao ambao
wanatarajia kuingia nchini hivi karibuni ataanzia kutoa huduma hiyo katika
hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza na kisha hospitali ya Rufaa ya mkoa
wa Dodoma.
Bw. Gulamali ametoa kauli hiyo Jumapili,
Oktoba 2, 2016 wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda hicho akiwa
kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.
“Mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa
moyo mara sita na Desemba atafanyiwa upasuaji mwingine nchini India. Nikiwa
nchini India nimefahamiana na kujenga urafiki na madaktari wengi wa moyo kati
yao 14 watakuja nchini na kutoa huduma ya matibabu hayo bure,”amesema.
Mbali na kupeleka madaktari hao
katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, pia Bw. Gulamali ameahidi
kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana magodoro mapya kwenye
hospitali hiyo.
Wakati huo huo Bw. Gulamali
amemkabidhi Waziri Mkuu magodoro 200 yenye thamani ya sh. milioni 10 kusaidia
wananchi waliathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 na
kusababisha vifo vya watu 17 wengine 440 walijeruhiwa.
Pia tetemeko hilo limesababisha
nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada
ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315
wakihitaji misaada mbalimbali.
Waziri Mkuu alishukuru Bw. Gulamali
kwa msaada huo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha magodoro hayo inayafikisha
Kagera kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.
Pia Waziri Mkuu alimpongeza
Mkurugenzi wa kiwanda hicho kwa uamuzi wake wa kuleta madaktari bingwa wa moyo
kutoka India watakaotoa huduma ya upasuaji kwa watoto ambao baadhi yao wazazi
wao hawana uwezo wa kuwapeleka nchini India.
“Pia nimefarijika kukuta kiwanda
chako kipo hai na kinafanya kazi nzuri ya kusalisha magodoro bora. Nakupongeza
kwa kutekeleza wito wetu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa kuajiri Watanzania
147 kati ya watumishi 150 walioajiriwa kiwandani hapa,” alisema.
Bw. Gulamali alisema anatarajia
kuwekeza katika ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti
kitakachogharimu sh. bilioni nne hivyo kitaongeza fursa ya ajira kwa
Watanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU
JUMAPILI, OKTOBA
02, 2016
No comments:
Post a Comment