Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa
katika baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, ikiwa
ni pamoja na mitandao ya kijamii vikizungumzia hali ya dawa nchini hasa
kufuatia taarifa zilizotolewa na taasisi ya kiraia na baadhi ya viongozi wa
vyama vya siasa.
Taarifa hizo zilidai kwamba katika
kipindi hiki kuna upungufu mkubwa wa dawa katika bohari kuu ya dawa , Hivyo,
kusababisha kukosekana kwa dawa katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Taarifa hizi si sahihi na zinalenga
kupotosha umma na kuwatia wananchi wasiwasi. Napenda kuwathibitishia wananchi
kuwa Afya ni suala la kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Hivyo,
ningependa kutoa ufafanuzi kwa wananchi katika masuala yafuatayo; –
Hali ya Upatikanaji wa dawa
Hali ya upatikanaji wa dawa kwa
sasa iko vizuri. Dawa muhimu zinazohitajika sana nchini zinapatikana
kwenye maghala ya Bohari ya Dawa (MSD). Mfano kwa upande wa dawa za antibiotics
tuna Amoxycillin, Ciprofloxacin, Cotrimoxazole na Doxycycline. Kwa upande wa
dawa za maumivu – tunazo za kutosha kama vile paracetamol, asprin na
diclofenac.
Pia tuna dawa za kutosha za
malaria, Kifua Kikuu, ukoma na dawa za kufubaza makali ya UKIMWI (ARVs). Kwa
upande wa chanjo za watoto na wajawazito, ni kweli kulikuwa na uhaba nchini kwa
kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Hata hivyo, wiki iliyopita Serikali
imenunua na kupokea dozi milioni 2 za chanjo ya Kifua Kikuu (BCG), dozi milioni
1.2 za Polio na dozi milioni za Polio. Chanjo hizi zinasambazwa katika vituo
vya afya nchini.
Dawa nyingine zitaendelea
kupatikana katika Bohari kuu ya Dawa kwa kuwa tumeagiza dawa za kutosha kutoka
kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, kiasi kikubwa cha dawa
zinazowasili Bohari kuu ya Dawa zikifika zinapelekwa kwenye Kanda nane za MSD
pamoja na vituo viwili vya Mauzo kwa ajili ya kuwasambazia wateja
walioagiza.
Hivyo, kipimo cha upatikanaji wa
dawa si kuangalia katika maghala ya Bohari ya Dawa peke yake bali pia katika
vituo vya kutolea huduma za afya.
Ili kuondoa mlolongo wa manunuzi ya
dawa, tunapenda kuwataarifu kuwa Bohari kuu ya Dawa imepanua wigo wa
upatikanaji wa dawa kwa sasa kwa kutumia mikataba ya muda mrefu (miaka miwili)
na washitiri wa ziada wa ndani (Prime Vendors) ili kuhakikisha dawa
zinapokosekana MSD zinapatikana kwa haraka kwa Washitiri wa ndani
waliothibitishwa katika kila mkoa.
Katika muktadha huo huo, Bohari ya
Dawa imefungua maduka ya ziada kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa dawa zaidi
ya aina 600 kupitia mfumo wa maduka katika mahospitali kama vile Muhimbili,
Mbeya na Arusha.
Bajeti ya dharura kwa ajili ya dawa
Ni muhimu wananchi wakajua kuwa
fedha zilizotengwa kwa ajili ya manunuzi ya dawa katika mwaka wa fedha 2016/17
zinatosha kuhudumia mahitaji ya dawa kwa mwaka mzima. Hivyo hakuna sababu ya
kuwa na bajeti ya dharura.
Niwakumbushe bajeti zilizotengwa
kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba katika miaka michache iliyopita mpaka
hivi sasa, kama ifuatavyo: -.
Mwaka 2011/2012 bajeti iliyotengwa
ilikuwa shilingi Bilioni 23.7
Mwaka 2012/2013 bajeti ilikuwa
shilingi Bilioni 34
Mwaka 2013/2014 ilikuwa shilingi
Bilioni 34
Mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi
Bilioni 60
Mwaka 2015/2016 ni shilingi Bilioni
30
Na mwaka huu 2016/17 ni shilingi
Bilioni 251.5
Mkakati wa Wizara kwa sasa ni
kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapatikana kwa wakati kutoka Hazina kulingana na
makusanyo ya nchi.
Vilevile ieleweke kwamba tayari
serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 20 katika kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17, kwenda Bohari kuu ya Dawa kwa ajili ya
ununuzi wa dawa na chanjo. Hali hii inathibitisha kuwa suala la upatikanaji wa
dawa ni la kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya tano.
Kulipa Deni la Bohari ya Dawa (MSD)
Napenda kuwafahamisha kuwa Serikali
imedhamiria kulipa deni lote la Bohari ya Dawa (MSD) ambapo katika mwaka huu wa
fedha 2016/17 tayari Bilioni 85 imekwishatenga kwa ajili ya kulipa deni
hilo.Jambo ambalo halijawahi kutokea huko nyuma. Kulipwa kwa deni hilo
kutasaidia kuhuisha mtaji wa MSD (revolving fund) na hivyo kuiwezesha MSD kuwa
na dawa na vifaa tiba kwa kiwango kikubwa.
Aidha serikali imekwisha kuviagiza
vituo vyote vinavyotoa huduma za Afya kupitia Halmashauri zao, kuhakikisha
zinakuwa na fedha ya mzunguko kwa ajili ya kununulia dawa (revolving fund) na
hivyo kupata dawa kwa kulipa fedha taslimu kutoka Bohari ya Dawa badala ya
kukopa.
Fedha hizo zitapatika kutoka kwenye
vyanzo vyao vingine vya mapato kama vile Bima ya Afya (NHIF, CHF) na gharama
wanazochangia wananchi katika kupata huduma. Hii itawezesha kutoendelea kukuza
deni kutoka Bohari ya Dawa na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati wote.
MSD Kupata Mshindani
Katika mwaka 2015, Serikali ilimpa
kazi mshauri mwelekezi wa kampuni ya ushauri iliyobobea kimataifa ya Deloitte
ya kulitazama jambo hili kwa ajili ya kuifanyia tathmini MSD pamoja na mambo
mengine ikiwemo kuangalia suala ya kutafutiwa mshindani katika manunuzi na
usambazaji wa dawa.
Napenda kuwajulisha kuwa tathmini
hiyo ilionyesha kuwa MSD kutafutiwa mshindani itakuwa ni kuongeza gharama kubwa
kwa serikali kutokana na kurudufisha (duplication) majukumu.
Pia ilibainika kuwa suala la dawa
ni muhimu, hivyo Serikali haiwezi kuliacha kwenye mikono ya watu binafsi.Jambo
ambalo lilipendekezwa ni kuifanyia maboresha makubwa MSD ili iweze kutekeleza
majukumu yake ipasavyo. Utekelezaji wa mapendekezo hayo tayari umeshaanza.
Nchi ambazo zinaiuzia dawa na vifaa
tiba MSD
MSD inaagiza dawa na vifaa tiba nje
ya nchi zaidi ya asilimia 80 kwa sababu viwanda vilivyoko ndani ya nchi
havikidhi mahitaji ya nchi kwa ubora na kiasi. Hivyo, MSD hununua dawa na vifaa
tiba kutoka nchi za India, China, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Ujerumani,
Marekani, Ufaransa na sehemu nyingine duniani.
Kwa mfano, tuna dawa zaidi ya
aina nne ambazo zinanunuliwa kutoka Kenya (Dawa ya kutibu malaria kwa
akina mama wajawazito ijulikanayo kama Sulfadoxine Pyrimethamine (SP), dawa ya
kutibu magonjwa ya maambukizi ya Cotrimoxazole ya watu wazima na watoto
pamoja, Amoxicilline na Paracetamol ya maji kwa ajili ya watoto.
Ikumbukwe kuwa MSD hununua dawa
hizi kupitia mchakato wa zabuni, ikiwa baadhi ya vigezo ni kuangalia usajili wa
dawa nchini pamoja na ushindani wa bei. Hata hivyo, ili kukuza viwanda vya
ndani, watengenezaji wa dawa wa ndani hupewa hadi 15% ya upendeleo katika
mchakato wa tathmini ya zabuni dhidi ya dawa zinazotoka nje ya nchi (Domestic
preference).
Kwa upande mwingine mkakati wa
serikali sio kuendelea kutegemea dawa kutoka nje ya nchi, kwani kwa kufanya
hivi uchumi wa nchi hautakuwa. hivyo basi serikali iko katika hatua za mwisho
za utaratibu wa kuwakaribisha wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha dawa kuwekeza
nchini kwa mpango wa kuwashirikisha wadau wengine katika masuala ya dawa
(PPP).
Hitimisho
Wizara ya afya inapenda
kuwahakikishia wananchi kuwa itasimammia ipasavyo utapatinaji wa dawa, vifaa na
vifaa tiba nchini kwa wakati na kwa bei nafuu kwa kuwa Sera ya afya inawataka
wananchi kuchangia huduma.
Aidha vituo vya kutolea huduma za
Afya vinahimizwa kupeleka mahitaji na maoteo yao ya dawa kwa wakati badala ya
kusubiri hadi dawa zote muhimu zimeisha kabisa katika vituo vyao. Pia
wanakumbusha kulipa madeni wanayodai na bohari ya dawa sambamba na kuhakikisha
fedha inayopatikana katika shughuli za utoaji huduma inatumika kwa ajili ya
dawa, vifaa na vifaa tiba.
Ili kuondoa vikwazo kwa
wananchi katika kupata dawa na huduma za afya kwa ujumla wananchi wanahimizwa
kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya kwani hakuna anayejua leo hama kesho ataugua
na Magonjwa hayapigi hodi na wakati mwingine yanakukuta hauna akiba ya
fedha, ila ukiwa na bima wakati wowote unapata matibabu.
Mwisho, Wizara itaendelea
kuhakikisha kuwa kuna dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara vya kutosha
kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za Afya nchini
No comments:
Post a Comment