Mwanamume mmoja amefariki wakati wa maandamano ya upinzani katika mji wa Kisumu, magharibi mwa Kenya, watu walioshuhudia wameambia BBC.
Mwanamume huyo anadaiwa kufariki wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji hao wanaowashinikiza maafisa wa Tume ya Uchaguzi (IEBC) kujiuzulu.
Hospitali moja mjini humo imethibitisha kwamba mwili wa mwanamume umefikishwa katika hospitali hiyo lakini chanzo cha kifo chake hakijathibitishwa.
Jijini Nairobi, maafisa wa polisi wametawanya waandamanaji waliokuwa wakitaka kufika katika afisi kuu za tume hiyo.
Shughuli za kibiashara katika jiji hilo zimetatizika pakubwa.
Polisi wamekuwa wakikabiliana na makundi ya wafuasi wa muungano huo wa upinzani wa Cord kwa mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha.
Maandamano pia yameshuhudiwa katika miji mingine kama vile Mombasa na Kakamega.
Leo imekuwa wiki ya nne ya maandamano hayo ya upinzani.
Wiki iliyopita, polisi walikabili vikali waandamanaji na baadaye walishutumiwa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa kutumia "nguvu kupita kiasi”.

No comments:
Post a Comment