Urusi imesitisha mkataba wake na
Marekani kuhusu kutupwa kwa madini ya ziada ya plutonium ambayo yanaweza
kutumiwa kuunda silaha, ishara ya kudorora kwa uhusiano kati ya mataifa hayo
mawili yenye ushawishi mkubwa duniani.
Kupitia agizo rasmi, Rais Vladimir Putin ameituhumu Marekani kwa
kuunda "kikwazo cha kutishia utathabiti, kwa kuchukua hatua zisizo za
kirafiki" dhidi ya Urusi.
Bw Putin alisema Urusi imelazimika kuchukua "hatua za
dharura kulinda usalama wa taifa la muungano la Urusi".
Moscow imetoa masharti ya kutimizwa na Marekani kabla ya
kurejelewa kwa mkataba huo.
Chini ya mwafaka huo wa mwaka 2000, kila taifa linapaswa
kuangamiza tani 34 za madini ya plutonium kwa kuyachoma kwenye vinu vyake.
Mpango huo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kupunguza silaha
za nyuklia.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema tani 68 za madini ya
plutonium ambazo zingeangamizwa "zinatosha kuunda silaha 17,000 za
nyuklia".
Pande zote mbili zilikuwa zimetia saini upya mkataba huo mwaka
2010.
Kwingineko, Marekani nayo imetangaza kwamba itasitisha
mazungumzo na Urusi kuhusu mzozo Syria.
Marekani imesema Urusi haijatimiza masharti yaliyoafikiwa chini
ya mpango wa kusitisha mapigano kwa muda mwezi jana, ambao umesambaratika.
Urusi imesema hatua hiyo ni ya kusikitisha na badala yake
ikailaumu Marekani kwa kujaribu kuiwekea lawama Urusi.
Bw Putin aliwasilisha mswada kwa bunge la taifa hilo ambao
unaeleza masharti yanayofaa kutimizwa na Marekani kabla ya kurejelewa kwa
mkataba huo wa madini ya plutonium.
Masharti hayo ni pamoja na:
§
Kupunguzwa kwa wanajeshi wa Marekani na silaha zake katika nchi
zilizojiunga na Nato baada ya 1 Septemba 2000
§
Kuondolewa kwa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Urusi na
kulipwa fidia kutokana na madhara yaliyotokana na vikwazo hivyo.
Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya waliiwekea Urusi vikwazo
kufuatia hatua ya Moscow ya kuchukua jimbo la Crimea kutoka kwa Ukraine mwaka
2014, pamoja na hatua ya Urusi ya kuunga mkono wapiganaji wanaotaka kujitenga
kwa maeneo ya mashariki kwa Ukraine.
No comments:
Post a Comment