Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) George Simbachawene amekuwa kiongozi wa pili kumhoji Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu mradi wa mabasi wa Udart. Jana Simbachawene alipotembelea mradi huo alimtaka Makonda kuweka askari wa kutosha watakaodhibiti uvunjwaji wa sheria katika mradi huo.
Huyo ni kiongozi wa pili kumhoji Makonda kuhusu mradi wa Udart, baada ya hivi karibuni Rais John Magufuli kumtaka asimamie kwa kutoa adhabu kali kwa wale watakovunja sheria kwenye mradi huo.
Katika ziara yake jana, Simbachawene alipanda gari nambari T121DGW kutoka Kimara mpaka Kiarikoo Gerezani na alipofika alipokelewa na Mkuu wa Mkoa, wakuu walaya na viongozi wengine.
Hata hivyo, aliwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa mpya kwa kujenga vituo vya maegesho ya magari karibu na stendi za mabasi ya haraka ili watu wanaotaka kwenda mjini wawe wanaegesha magari yao na kupanda mabasi hayo, ambako mbali na kuwahi kazini wataokoa gharama za mafuta.
Katika hatua nyingine; Simbachawene amepiga marufuku ombaomba na wafanyabiashara maeneo ya mjini na kumtaka Makonda kutekeleza maagizo hayo kwa kuweka askari wa kuwaondoa.
Alisema watu wanaowapa ombaomba pesa siyo kwamba wana mipango mizuri na Serikali kwa kuwa watoto wanaotumika kuomba walitakiwa wawe shule.
Makonda alisema kuwa utekelezaji wa maagizo hayo umeanza mara moja, kwani yaliyotolewa yapo kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Makonda alisema kuwa ana mpango wa kuongeza muda wa kufanya biashara katika maduka makubwa na katika soko la Karikaoo kuwa mpaka saa nne za usiku.
No comments:
Post a Comment