
SERIKALI imetoa siku 30 kukamatwa
kwa watumishi waliosababisha matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii Tanzania (TASAF) III, kwa kuingiza majina ya watu masikini wasiostahili
ili kujipatia fedha za mradi huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene
akizungumza na baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi, jana alisema ni
lazima watumishi wa umma waliohusika katika kuisababishia hasara Serikali wawajibishwe.
Februari mwaka huu, TASAF
ilitekeleza maagizo ya Serikali na kufanya uhakiki wa kaya masikini ziliopo
kwenye mpango wa kupata fedha na kuziondoa zile zilizokosa sifa na kuziondoa
kaya 32,456.
“Katika msako huo tulibaini,
waliokufa ni 7,819, viongozi waliojipachika 2,999, waliohama sehemu ambapo
mpango haujaanza 3,948, wasiojitokeza au wasiofahamika 9,342 na wasiokuwa na
sifa 8, 348,”alisema Simbachawene.
Aidha alisema kuwa, zoezi hilo ni
endelevu na kwamba utaratibu wa kutoa taarifa za walengwa waliofariki au kuhama
unapaswa kufanyika ili fedha za serikali zisitumike ovyo nje ya malengo
yaliyokusudiwa.
Simbachawene alisema, kuingizwa
kaya zisizo na sifa katika mpango huo na kuachwa kwa kaya ambazo ni maskini
zaidi, kumetokana na baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao pia wamekuwa
wakipunguza malipo ya walengwa.
Watu 6.5 milioni, katika kaya
maskini na zinazoishi katika mazingira hatarishi wanatarajiwa kunufaika na
mradi wa fedha za TASAF katika awamu ya sasa.
Hata hivyo, Simbachawene
aliwashauri wakurugenzi wa halmashauri zote nchini pamoja na wakuu wa wilaya,
kutoogopa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
zilizopo kwani suala hilo litaepusha hasara na mianya ya wizi.
Mhandisi Evarist Ndikilo, Mkuu wa
Mkoa wa Pwani, alimuahidi waziri Simbacahwene kuwa, hawatofumbia macho
ubadhirifu katika halmashauri na kusema watazishauri, kuzikumbusha na hata
kuingilia kati pale mambo yanapoenda ndivyo sivyo katika halmashauri.

No comments:
Post a Comment