
Siku moja baada ya Chadema
kutangaza safu ya Ukuta, viongozi wa chama hicho wameanza kutawanyika mikoani
kuanza kutoa elimu ya mpango huo.
Wakati mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe akiwa Kanda ya Kaskazini aliyekuwa mgombea urais wa Chadema,
Edward Lowassa alikuwa mkoani Mbeya na jana alishiriki ibada na kuanza vikao
vya mkakati huo.
Mbowe jana alikutana na viongozi wa
kanda hiyo na kuunda kamati zitakazokwenda katika majimbo yote 35 ya uchaguzi
katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara kutoa elimu.
Mbowe alisema katika kikao hicho,
ambacho ni mfululizo wa vikao vinavyoendelea kanda zote nchini, wamekubaliana
kutoa elimu ya dhana ya Ukuta.
Hata hivyo, alisema bado chama
hicho kimetoa fursa ya mazungumzo kwa taasisi yoyote ili kuhakikisha mgogoro
uliosababisha Kamati Kuu kuunda Ukuta.
Wakati Mbowe akisema hayo, Lowassa
ametua katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayojulikana kama Kanda ya Nyasa
akiwa na mambo matatu makubwa.
Aliwasili jana asubuhi kwa ndege ma
kwenda moja kwa moja kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Usharika wa Forest akiwa na viongozi wa chama hicho wa kanda pamoja na wabunge
mbalimbali wa majimbo ya mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Songwe, Rukwa na wale
wa viti maalumu.
Waziri Mkuu huyo wa zamani,
alishiriki ibada ya kawaida na alipokea zawadi ya nyimbo zilizowekwa kwenye
‘flash’ kutoka kwa wanakwaya wa kanisa hilo huku naye akiwachangia kwa
kuendesha harambee ya papo kwa papo kutoka kwa viongozi alioongozana nao.
Katika harambee hiyo, zilipatikana
Sh4 milioni zikiwamo Sh 1 milioni ambazo aliahidi kuzitoa.
Kabla ya ibada kumalizika, Lowassa
na ujumbe wake waliondoka kwenda kwenye kikao cha Baraza la Chadema la
Kanda.
Katibu wa Kanda hiyo, Frank
Mwaisumbe alitaja mambo matatu makubwa kutoka kwa Lowassa kuwa la kwanza
alihimiza wanachama wote kuimarisha umoja na kufuta mipasuko iliyotokea wakati
wa uchaguzi.
Pili, aliwasihi wana Chadema wote
kuwa jasiri kwa kupigania haki na kujitambua na la tatu ni kujiandaa kwa
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 2019 na Uchaguzi Mkuu wa
2020.
Mwaisumbe alisema baada ya kikao
cha jana, leo Lowassa anaanza kutembelea majimbo ambako atakuwa na vikao vya
ndani katika majimbo ya Mbeya Vijijini, Mbozi na Tunduma na kesho atakuwa
kwenye majimbo ya Nkasi Kaskazini na Kusini na Sumbawanga wakati kesho kutwa
atakuwa Mbarali, Makambako, Njombe Mjini na Mafinga. Agosti 25 atakuwa Iringa
Mjini na Kolo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent
Mashinji yupo Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa mitatu; Simiyu, Shinyanga
na Mara na jana aliwataka Watanzania kuwapuuza watu wanaodai chama hicho
kimejipanga kufanya vurugu Septemba Mosi akisisitiza kuwa maandamano yatakayofanyika
ni ya amani.
Alisema kamwe hawawezi kuvunja
sheria na Katiba ya nchi na kwamba kinachofanyika kipo kwa mujibu wa sheria.
“…Nawaomba Watanzania wote
watuunge mkono maana tunachokwenda kukifanya ni kwa ajili ya kuwanusuru watoto
wetu wasiingie kwenye matatizo maana kinachoendelea kinakwenda kuondoa
demokrasia na utawala bora,” alisema.

No comments:
Post a Comment