Wapo niliowasiliana nao na kuonyesha
kutofahamu vizuri ni siku zipi ambazo ni za hatari au kwa namna nyingi zile
siku ambazo ni zakuweza kupata ujauzito.
Njia ya
kalenda ni moja ya njia ambazo wenye kushikilia mila na desturi na imani za
kidini hupendelea kuitumia njia hii ya asili ili kufanya uzazi wa mpango.
Njia ya
kalenda ni njia inayohitaji nidhamu kwa wenza wawili na pia inahitaji kujifunza
na kuizoea angalau kuifanyia mazoezi kwa muda wa miezi 3-6 vinginevyo njia za
vidonge, vipandikizi na sindano ndio zinafanikiwa kukukinga usipate ujauzito.
Wapo
waliokuwa wanadhani ujauzito unaweza kupata siku inayofuata baada damu ya hedhi
kukata, mwingine alikuwa akijua kuwa kuifahamu siku ya hatari ambayo yai
limekomaa tayari zinahesabiwa kutoka mara ya mwisho damu ya hedhi kuisha.
Kawaida
wanawake walio wengi duniani kwa mujibu wa machapisho mbalimbali ya kitafiti ya
kisayansi mzunguko wa hedhi wa kawaida ni siku 28-30 karibu asilimia 85-90.
Ingawa
wapo wachache ambao wana mzunguko mfupi wa siku 21 na wapo wenye mzunguko wa
mrefu wa hedhi wa siku 35-42.
Mwanamke
hupata hedhi kipindi ambacho kama mimba haikutungwa ngozi nyororo iliyomo
katika mfuko wa uzazi hunyofoka na kutolewa nje kama damu ya hedhi.
Katika
mzunguko wa hedhi kipo kipindi maalumu ambacho kiyai cha kike huwa tayari
kimekomaa na endapo kitakutana na mbegu ya kiume mimba huweza kutungwa.
Kipindi
hiki huwa ni siku ya 14 kwa wanawake walio wengi ambao mzunguko wao ni siku 28,
huhesabiwa tangu siku ya kwanza lilipotoka tone la damu ya hedhi na sio siku ya
mwisho hedhi ilipokata.
Ili
kuweza kujua siku za mimba kutungwa inakubidi kuhesabu siku ya kwanza kupata
hedhi mpaka siku ya 14 kwa wale wanawake wenye mzunguko siku 28.
Kwa
kawaida wanawake wote hata kama wana mizunguko ya hedhi ina urefu wa siku isiyo
sawa zile siku za matayarisho yai kutengenezwa huwa ni sawa ambazo huwa ni siku
14.
Ili
kuweza kujua siku yako ya kuweza kupata ujauzito unachukua siku 14 unatoa kwa
siku za mzunguko wako. Kwa mfano, kama wewe uliyeuliza swali mzunguko wako ni
siku 30 unatoa kwa 14, hivyo unapata 16.
Hivyo
yai lako linakuwa limekomaa na kuweza kurutubishwa na mbegu ya kiume katika
siku ya 16. Nitoe mfano mwingine; tuchukulie una mzunguko wa mfupi ambao ni
siku 21 ili kujua siku yako hasa ya yai kuwa limekomaa unatoa siku 14 hivyo
unapata 7.
Mtu
mwenye mzunguko wa siku 21 yai lake linakuwa limekomaa siku ya 7. Kwa wenye
mzunguko wa siku 28 ambao ndiyo wengi unachukua 14 unatoa 28 unapata siku 14.
Ndiyo
maana inazungumzwa kuwa siku ya 14 ndiyo siku ya hatari kwa wanawake wengi ndio
maana wanaiepuka bila kujua pia mwenye mzunguko wa siku 28 pia ana nafasi ya
kupata katika siku ya 11, 12, 13, 15, 16, 17 na 18.
Hivyo
basi ili kuweza kuondoa uwezekano wa kupata ujauzito unaweza kutumia kanuni ya
kujumlisha siku 3 au kutoa 3 pale unapojua siku yako ya hatari. Ingawa wengine
huamua kutumia kujumlisha au kutoa 4.
Kwa yule
aliyeuliza swali ambaye ana mzunguko wa siku 30, ambaye tumejua kuwa siku yake
yai kuwa limekomaa tayari ni siku ya 16. Hivyo tukijumlisha siku 3 tunapata
siku 17, 18, 19 wakati tunapotoa siku 3 tunapata siku ya 15, 14, 13.
Hivyo
basi siku zako za hatari ambazo unaweza kujikuta unapofanya tendo bila kinga
yoyote ya uzazi wa mpango unaweza kupata ujauzito ni siku ya 13-19 (Kwa mwenye
mzunguko wa siku 30).
Ingawa
ni kweli kuwa siku ya kuweza kupata ujauzito hasa ni moja lakini zipo siku
ambazo pia zinakuwa na nafasi ya kuweza kupata ujauzito, ambazo huwa tunaziita
siku za hatari kitabibu huitwa unsafe days.
Kwa kuwa
yai la kike huwa na uwezo wa kurutubishwa na kuwapo kwa muda wa saa 24-78,
mbegu za kiume huwa na uwezo wa kuwa hai kwa saa 24-48.
Hivyo
basi kama utakutana na mwenza wako siku ya 11, 13 au 15, 16 unaweza kupata
ujauzito. Kwa mfano, kama utakutana na mwenza siku ya 16 na yai la kike likiwa
limekomaa siku ya 14 kuna nafasi ya kupata ujauzito kwa sababu kiyai cha kike
linaweza kuwa hai kwa siku moja mpaka tatu.
Vilevile
kama utakutana na mwenza wako siku ya 12 wakati kiyai cha kike bado siku mbili
kukomaa, nafasi ya kupata ujauzito ni kubwa kwa sababu mbegu ya kiume huwa na
uwezo wa kuwa hai kwa siku mbili, hivyo itakapokutana na yai siku ya 14 mimba
hutungwa.
Zipo
dalili ambazo hujitokeza ambazo huashiria kuwa yai la kike huwa tayari
limekomaa na mimba kuweza kutungwa. Dalili ni kama vile ute wa uke huwa mzito
na mwingi ukilinganisha ni siku za kawaida.
Endapo
utavuta na kidole gumba na kidole cha shahada huwa ute huo haukatiki, ute huo
huwa na rangi kwa mbali kama vile kutu. Joto la mwili huwa juu.
Matiti
na upande wa kulia chini ya tumbo huuma kwa mbali, kujihisi hamu ya kufanya
tendo la ndoa, pia kuna uthibitisho kuwapo kwa harufu fulani maalumu ambayo
humpa msisimko mwanaume.
No comments:
Post a Comment