Uingereza imetoa mchango wa
Shilingi Bilioni 6 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa
miundombinu ya shule zilizopata madhara kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea
katika Mkoa wa Kagera tarehe 10 Septemba, 2016.
Mchango wa fedha hizo umewasilishwa
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Balozi
wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Catherine Cooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam
muda mfupi baada ya Balozi huyo kuwasilisha hati zake za utambulisho.
Balozi Sarah Catherine Cooke
amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kutoa mchango wa fedha hizo Waziri Mkuu
wa Uingereza Mhe. Theresa May anatoa pole kwa Serikali ya Tanzania na kwa
familia zote zilizopatwa na madhara ya tetemeko hilo na kwamba Uingereza imeona
ishirikiane na Tanzania katika kukabiliana na madhara hayo.
“Uingereza imeguswa sana na maafa
yaliyowakumba wananchi kufuatia tetemeko lililotokea Kagera, tunapenda kuona
wananchi wanasaidiwa na wanafunzi wanaendelea na masomo” amesema Balozi
Sarah Catherine Cooke.
Kwa Upande wake Rais Magufuli
amemshukuru Waziri Mkuu wa Uingereza kwa mchango huo ambao utasaidia juhudi za
Serikali za kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule.
“Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke
naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe.
Theresa May na umueleze kuwa kwa niaba ya watanzania hususani waliopatwa na
madhara ya tetemeko la ardhi tumeguswa sana na moyo wake wa upendo kwetu” amesema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli na Balozi Sarah
Catherine Cooke pia wamezungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya
Tanzania na Uingereza ambapo Rais Magufuli ametoa wito kwa Balozi huyo
kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Uingereza kuongeza uwekezaji
wao hapa nchini na kwamba Tanzania itaendeleza na kukuza uhusiano huo.
“Uingereza ni rafiki na ndugu wa
kweli na wa kihistoria kwa Tanzania, tunatambua kuwa nchi yenu ni mdau mkubwa
na muhimu wa maendeleo yetu, hivyo tusingependa kupoteza rafiki na ndugu yetu,
tuendelee kushirikiana kwa manufaa ya wananchi.
“Natambua kuwa Uingereza ina
utaalamu mkubwa katika masuala ya gesi hivyo nawakaribisha waje wawekeze katika
sekta ya gesi”amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema
Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia kukabiliana
na madhara ya maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera zinafikishwa
kwa walengwa na ameonya kuwa watakaothubutu kuiba fedha hizo watashughulikiwa.
Dkt. Magufuli amebainisha kuwa
baada ya kutengua uteuzi na kuchukua hatua nyingine dhidi ya aliyekuwa Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius Msole na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba
Bw. Steven Makonda pamoja na kumsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Bw. Simbaufoo Swai, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles
Kimei awachukulie hatua watumishi wa Benki hiyo walioshirikiana na watumishi
hao kufanya njama za kuanzisha akaunti nyingine ya benki yenye jina
linalofanana na akaunti rasmi ya “Kamati ya Maafa Kagera” kwa lengo la
kujipatia fedha”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
28 Septemba, 2016
No comments:
Post a Comment