Baraza la Usalama la umoja huo limetoa wito kwa wagombea wakuu
na wafuasi wake kujizuia kufanya uchokozi na kutatua mzozo wa sasa kupitia njia
za kisheria.
Maafisa wa usalama kufikia sasa wamewakamata watu zaidi ya elfu
moja baada ya siku ya pili ya maandamano ya wafuasi wa upinzani.
Upinzani unadai Rais Ali Bongo aliiba kura wakati wa uchaguzi
huo uliofanyika Jumamosi.
Watu watatu waliuawa mji mkuu Libreville.
Rais Bongo amesisitiza kwamba alishinda kwa njia halali
na kuutaja ushindi wake kuwa ushindi wa watu wa Gabon.
Amesema kuna kundi ndogo la watu
wachache waliotaka kutwaa madaraka na ambao wameshindwa.
Matokeo ya uchaguzi yalitangazwa
Jumatano alasiri na kumpatia Bw Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura, akifuatwa na
Bw Ping aliyepata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.
Bw Ping alisema uchaguzi huo ulijaa
udanganyifu na "hakuna ajuaye" hasa nani alishinda.
Upande wa Bw Ping unasema takwimu kutoka ngome za rais
huyo zinaonyesha asilimia 99 ya wapiga kura walijitokeza. Ameomba takwimu za
wapiga kura kutoka kila kituo zitolewe wazi.
Bw Bongo aliingia madarakani mwaka
wa 2009, baada ya kifo cha babake aliyekuwa ameongoza taifa hilo tangu 1967.
Kabla ya kuingia katika siasa, Ping
aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

No comments:
Post a Comment