TAMKO LA BODI YA WADHAMINI YA THE
CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) KUFUATIA KIKAO CHAKE
KILICHOFANYIKA JANA, TAREHE 2 OKTOBA, 2016
Kwa kuzingatia hali iliojitokeza
katika chama chetu cha THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
kufuatia hatua ya makusudi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi, kutupandikizia vurugu na fujo kwa kujipa mamlaka asiyokuwa nayo ya
kutuamulia nani awe Mwenyekiti wa Chama, hatua ambayo imesababisha mtu
anayeitwa Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake tarehe 24 Septemba, 2016 kuvamia
na kuhodhi jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, Bodi ya
Wadhamini ya Chama iliona kuna haja ya kukutana na kuchukua hatua za
kukabiliana na matukio hayo.
Bodi ya Wadhamini ya The Civic
United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) imefanya kikao chake, tarehe 2 Oktoba,
2016 katika Makao Makuu ya Chama, mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Mhe.
Abdallah Said Khatau.
Tumefanya hivyo kwa kutambua wajibu
wetu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258 ya Sheria za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (Political Parties Act, Cap 258) na Katiba ya CUF ya 1992
(Toleo la 2014).
Ni vyema ieleweke kwamba kwa mujibu
wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu
kinapaswa kuunda Bodi ya Wadhamini ambayo ndiyo inayokuwa mmiliki na msimamizi
wa mali zote za chama cha siasa husika. Kifungu cha 21 cha Sheria ya Vyama vya
Siasa kinalieleza hilo kama ifuatavyo:
“21. —(1) Every political party
which has obtained a certificate of full registration shall appoint a board of
trustees to manage the properties and any business or investment of the party.
(2) Every board of trustees shall
be duly incorporated under the Trustees Incorporation Act and every party
shall, not later than sixty days from the date of full registration, submit to
the Registrar—
a) the names and addresses of the
members of ther board of trustees; and
b) a copy of the certificate of incorporation.”
CUF kilitimiza masharti hayo ya
kisheria kwa kuunda Bodi ya Wadhamini, na Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la
2014), Ibara ya 98 ikafafanua zaidi namna inavyopatikana, pamoja na nguvu na
uwezo wake kichama, kama ifuatavyo:
“98._ (1) Kutakuwa na Bodi ya
Wadhamini ya Chama itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu
wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa
tena baada ya muda wake kumalizika.
(2) Bodi itakuwa na wajumbe
wasiozidi tisa (9), watano (5) kutoka Bara angalau wawili (2) wakiwa ni
wanawake na wanne (4) kutoka Zanzibar angalau mmoja (1) akiwa ni mwanamke ambao
watateuliwa kwa masharti yanayohitajika ya Sheria ya Bodi ya Wadhamini na utaratibu
uliowekwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
(3) Bodi ya Wadhamini itakuwa ndiyo
mdhamini pekee wa fedha na mali za Chama pamoja na madeni na itafanya shughuli
zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na sheria ya nchi inayohusu
Wadhamini.
(4) Bodi inaweza kushitaki au
kushitakiwa kwa niaba ya Chama.
(5) Bodi itawajibika kwa Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa la Chama ambalo linaweza kuweka utaratibu unaofaa wa
kuendesha shughuli za Bodi hiyo, na itafanya vikao vyake angalau mara mbili kwa
mwaka.
(6) Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini watachaguliwa na Wajumbe wa Bodi kutoka miongoni mwao, kwa
sharti kwamba Mwenyekiti akitoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Naibu
Mwenyekiti atatoka upande mwengine wa Jamhuri ya Muungano.”
MAAMUZI YA BODI YA WADHAMINI:
Kufuatana na uwezo wake uliotajwa
hapo juu na kwa kuzingatia nafasi yake kama mdhamini pekee wa fedha na mali za
Chama (rejea Ibara ya 98(3) iliyotajwa hapo juu, Bodi ya Wadhamini imefikia
maamuzi yafuatayo:
1. Imepuuza wito wa mtu anayeitwa
Ibrahim Haruna Lipumba alioutangaza jana kwamba eti amemtaka mtu mwengine
anayeitwa Thomas Malima kuitisha kikao cha Bodi ya Wadhamini. Lipumba kwa sasa
si Mwenyekiti tena wa CUF na pia si mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa
uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
2. Itaendelea kuwajibika kwa Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la Chama kama inavyotakiwa na Ibara ya 98(5) ambalo
ndilo linaloiteua Bodi na litaheshimu maamuzi yote ya Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa likiwa ndiyo chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa
Chama.
3. Itachukua hatua za kisheria
chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(3) na 98(4) kurejesha chini ya
dhamana yake mali zote za Chama zilizovamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Ibrahim
Lipumba na genge lake ikiwemo jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar
es Salaam.
4. Itachukua hatua za kisheria
chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kumtaka
alipe gharama na hasara zote alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalum
wa Taifa wa Chama, tarehe 21 Agosti, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo
Plaza na genge lake kufanya vurugu, ghasia na uharibifu wa mali za hoteli na
hatimaye kuvuruga Mkutano Mkuu jambo lililosababisha hasara ya takriban Sh. 600
milioni; na kisha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam, tarehe
24 Septemba, 2016 ambapo alisababisha hasara ya takriban Sh. 50 milioni.
5. Itachukua hatua za kisheria
chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) kwa kumshtaki Msajili wa Vyama
vya Siasa kwa kuingilia maamuzi halali ya vikao halali vya Chama na kulazimisha
kukichagulia Chama chetu Mwenyekiti kinyume na onyo lililowahi kutolewa na
Mahakama Kuu dhidi ya Ofisi yake kutokuwa na mamlaka ya aina hiyo.
6. Inawahakikishia wanachama wote
wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar kwamba Bodi yao ya Wadhamini iko makini na
itasimama pamoja nao kulinda mali zote za Chama.
7. Inaionya Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa iwache kuingilia mambo ya ndani ya uongozi na uendeshaji wa
Chama cha CUF.
HAKI SAWA KWA WOTE
Abdallah Said Khatau
MWENYEKITI WA BODI
Joran Lwehabura Bashange
KATIBU WA BODI
No comments:
Post a Comment