Watu sita wameuawa baada ya watu wenye
silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia eneo lenye nyumba
za makazi Bulla usiku wa manane.
Gavana wa jimbo la Mandera Ali Roba ameandika kwenye Twitter
kwamba watu 6 wameuawa na mmoja kujeruhiwa.
Amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye ploti hiyo
wameokolewa na maafisa wa usalama.
Kituo kimoja cha redio kinachohusishwa na kundi la al-Shabab
kimesema wanamgambo hao ndio waliotekeleza shambulio hilo.
Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa watu walioshambuliwa
walikuwa "watu wa kutoka maeneo mengine".
Gazeti la Standard nalo linasema walioshambuliwa walirusha
guruneti kwanza na kisha wakaingia ndani na kufyatulia risasi waliokuwemo.
Bw Roba alisema dalili zote zinaashiria wavamizi hao walikuwa wa
kundi la al-Shabab.
Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na
wapiganaji wa al-Shabaab kutoka Somalia.
Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa
2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali
inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Kundi la al-Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulio nchini
Kenya ikiwemo mauaji ya watu 67 katika maduka ya Westgate mjini Nairobi mwaka
wa 2013.
Mwezi Juni mwaka huu, wanamgambo wa
kundi hilo walishambulia gari ya polisi aina ya Land Cruiser kilomita chache
kutoka mji wa Mandera, na kuua maafisa watano wa polisi.
Mwaka uliopita
al-Shabab walitekeleza mashambulizi katika chuo kikuu cha Garissa na
kusababisha vifo vya wanafunzi 148
No comments:
Post a Comment