Ofisa mdhamini wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Ali Mohammed Dadi amesema mshindi wa uwakilishi katika Jimbo la Ziwani ni Suleiman Ali wa CCM na si Asaa Hamad wa UPDP aliyetangazwa awali.
Dadi kutoka ofisi ndogo ya Pemba alisema jana kuwa msimamizi wa uchaguzi katika Wilaya ya Chakechake, Othman Hamisi alikosea wakati wa kujaza karatasi ya matokeo ya mshindi wa jimbo hilo.
“Nimezungumza naye na amesema kwamba alitoa ufafanuzi kuwa walifanya makosa katika kuandika matokeo, hivyo aliyeshinda ni mgombea wa CCM,” alisema.
Katika karatasi hiyo ya matokeo iliyokuwa imebandikwa ukutani, Asaa Ali Hamad alionekana kuwa amepata kura 221 dhidi ya 121 za mgombea wa CCM, lakini kwa ufafanuzi huo wa ZEC hakuna chama cha upinzani kilichoshinda nafasi ya uwakilishi au udiwani.
Kwa matokeo hayo, CCM imeshinda majimbo yote ya uwakilishi Unguja na Pemba na hivyo kuzidisha utata kwa Rais mteule, Dk Ali Mohamed Shein anayeapishwa leo, kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mujibu wa ibara ya 9 (3) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010.
Awali, kulikuwa na uwezekano wa UPDP kutoa mteule wa nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais kwa kuwa kilitangazwa kimakosa kupata kiti cha uwakilishi baada ya CCM lakini baada ya ufafanuzi huo wa ZEC matumaini hayo yameyeyuka.
Kuyeyuka kwa ndoto hiyo ya UPDP kunamaanisha kwamba hakuna chama kilichoshika nafasi ya pili kwa kupata kura asilimia 10 au zaidi, ambacho kwa mujibu wa Katiba hiyo kingekuwa na nafasi ya moja kwa moja kutoa makamu wa kwanza wa rais na baadaye mawaziri wa upinzani kuunda SUK.
Tangu Dk Shein atangazwe kushinda urais katika uchaguzi wa marudio baada ya matokeo ya ule wa awali kufutwa, mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii umekuwa ni jinsi gani atateua Serikali yake kukidhi matakwa ya Katiba ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya CCM na CUF kabla ya uchaguzi wa 2010.
Wakati Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akisema Rais Shein atatumia busara zake kumpata makamu wa kwanza wa rais, baadhi ya wanasheria wamesema hawaoni ufumbuzi wa moja kwa moja kutokana na upungufu huo wa kikatiba.
Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, Rais atateua makamu wa kwanza wa Rais kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili na mgombea wake wa urais kupata asilimia 10 ya kura za urais, au nafasi ya makamu wa kwanza itaenda kwa chama chochote cha upinzani kilichoshika nafaso pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
No comments:
Post a Comment