Mlipuko mkubwa ulitokea katika bweni la wanafunzi nambari D Jumatano jioni na baadhi ya wanafunzi waliodhani lilikuwa shambulio la kigaidi walikimbia, baadhi wakiruka kutoka vyumba vyao kupitia madirisha.
Chuo hicho kinasema mlipuko huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Wanafunzi katika bweni jirani nambari G ambao hawakufahamu kuhusu hitilafu hiyo walijawa na wasiwasi hasa baada ya mwanafunzi mmoja kusema “Al-Shabaab” kwa sauti.
“Wanafunzi waliojawa na wasiwasi waliruka kupitia madirisha kujiokoa. Wanafunzi watatu kutoka bweni D na 19 kutoka Bweni G waliumia,” chuo hicho kilisema kupitia ujumbe kwenye Facebook.
"Wanafunzi 11 kati ya hao wamepelekwa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret kwa matibabu zaidi. Hao wengine walitibiwa katika zahanati chuoni na kuruhusiwa kuondoka.”
Mlipuko huo ulitokea mwendo wa saa kumi na mbili kasoro dakika ishirini jioni.
Aprili mwaka jana, wanafunzi 147 waliuawa katika Chuo Kikuu cha Garissa, mashariki mwa Kenya baada ya wanamgambo wa al-Shabab kushambulia chuo hicho.
Chuo hicho kilifunguliwa tena Januari mwaka huu.
No comments:
Post a Comment