Serikali za Tanzania na Uganda zinatarajia kuanzisha mradi wa uwekezaji wa ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta unaolenga kuongeza pato la taifa na uchumi wa nchi hizo.
Mradi huo unatarajia kugharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni nne na utekelezaji wake utaanza mwanzoni mwa mwaka 2017.
Kauli hiyo imetolewa jana Jumatatu (Machi 28, 2016) Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wake na wafanyabiashara wa sekta ya mafuta nchini.
Prof. Ntalikwa alizitaja fursa ambazo zitanufaisha taifa kuwa ni pamoja na kodi zitakazolipwa, kuongezeka kwa wigo wa ajira kupitia miradi huo pamoja na tenda mbalimbali zitakazotolewa wakati na baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo.
“Tanzania ina kila sababu ya kupata mradi huo kwa kuwa ina uzoefu wa kuwa na mabomba kama hayo manne nchini na tunajivunia bandari yetu ya Tanga yenye kina kirefu kuliko bandari zote Afrika Mashariki”alisema Prof. Ntalikwa.
Prof. Ntalikwa alisema kuwa mwitikio wa wafanyabishara wa sekta ya mafuta nchini ni mzuri na kubainisha kuwa wanatarajia kusafiri kuelekea nchini Uganda kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana nchini humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa sekta ya mafuta nchini Dkt. Gideon Kaunda alisema kwa upande wao wataitumia vyema fursa ya uwekezaji katika ujenzi wa mradi huo na kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Imeandaliwa na Eleuteri Mangi-MAELEZO
No comments:
Post a Comment