Mtoto George Elias (7) amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya katani katika Kijiji cha Buganzu, Kata ya Uyovu wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita, tukio linalodaiwa kusababishwa na michezo ya kitoto.
Baba wa mtoto huyo, Elias Martin alisema mwanawe alikuwa anasoma darasa la awali katika shule ya msingi ya kijiji hicho na siku ya tukio alikwenda kucheza na watoto wenzake.
Martin alisema akiwa nyumbani kwake akipata chakula cha mchana na wageni waliokwenda kumtembelea, walifika watoto watatu wa jirani yake wakidai mtoto wake ananing’inia juu ya mti.
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo aliambatana na wageni wake mpaka eneo la tukio na kumkuta mtoto huyo akining’inia kwenye mti uliopo pembeni ya nyumba yake.
Mzazi huyo alisema chanzo cha tukio hilo ni michezo ya watoto na huenda alidanganywa na wenzake kuweka shingo kwenye kamba walipokuwa wakicheza.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Matayo Paschal alisema kuwa alipokea taarifa ya kifo hicho na kulijulisha Jeshi la Polisi.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Mpojoli Mwabulambo alisema wamefungua jalada la uchunguzi kuhusu tukio hilo, lengo likiwa kujua chanzo cha kifo hicho.
No comments:
Post a Comment