SERIKALI imesema imedhamiria kurejesha heshima ya wazee wote hapa nchini kwa kuisimamia jamii kuwathamini wazee na kuwapa kipaumbele katika huduma zote za jamii.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Mzee Kwanza inayolenga kuwapa kipaumbele wazee katika huduma zote za kijamii.
“Nataka heshima ya wazee irudi...wapate huduma kwa kupewa heshima yao, ifike mahali mzee anapofika sehemu yoyote akihitaji huduma apewe kipaumbele, ni lazima tuwape heshima yao kwa sababu wameifanyia nchi mambo makubwa wakati wa ujana wao,”alisema Waziri.
Alisema kuwa wazee katika jamii yoyote wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa kwa kuwa wao ni hazina ya busara, hekima, amani na utulivu wa jamii yoyote.
“Familia isiyoheshimu wazee aghalabu itakuwa na vurugu na ugomvi kila kukicha. Lakini jamii au familia inayoenzi wazee na kuwapa nafasi zao katika kushauri, kukosoa na kuelekeza utendaji wa siku hadi siku, jamii au familia hiyo itakuwa na baraka siku zote hivyo nikiwa Waziri mwenye dhamana nitahakikisha hili linawezekana,” alisema Waziri Ummy.
Alisema kuwa Serikali imeona ni vyema kurejea kwenye desturi hii kwa kuanzisha kampeni maalumu ya Mzee Kwanza ambaypo ni wajibu wa kila Mtanzania kuona kuwa anafanya kila awezalo kurejesha hadhi ya wazee na kuwapa umuhimu wa kwanza katika kupata huduma za kijamii.
Waziri Ummy alisema kuwa takwimu za sensa za mwaka 2012 zinaonesha kuna jumla ya wazee 2,507,568 wenye miaka kati ya 60 na kuendelea huku kukiwa na wazee takriban 474,053 wenye miaka 80 na kuendelea.
Alisema kuwa ili kuhakikisha wazee wanakuwa kwenye mazingira mazuri, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeandaa Muswaada wa kutungwa kwa Sheria ya Wazee ambayo itapelekwa Bungeni ili ipitishwe kuwa Sheria ambayo itasimamia upatikanaji wa haki na ustawi wa wazee Sheria hii itatoa ahueni kubwa kwa wazee na kuboresha sana maisha yao ya uzeeni.
Aidha alisema kuwa Serikali imeagiza kila halmashauri kubaini wazee walio katika maeneo yao na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na huduma za afya kutoka kwenye mapato yao wenyewe.
Akizungumzia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya aliupongeza kwa mwitikio waliochukua kushirikiana na Wizara katika Uzinduzi wa kampeni ya Mzee Kwanza katika huduma kwa nchi yetu.
“Najua hamasa hii wameipata kutokana na ukweli kwamba Mfuko huu unawahudumia wanachama wastaafu ambao nao wako katika kundi hili la wazee, nawapongeza NHIF kwa hatua mliyochukua ya kufanya mkutano na wanachama wenu wastaafu wiki chache zilizopita,”alisema.
No comments:
Post a Comment