Miaka minane iliyopita nilikutana na Haji Noorah Mwanza. Ilikuwa ni katika miaka yangu ya mwanzo mwanzo ya kama mtangazaji wa Radio Free Africa. Bado nilikuwa bwana mdogo kiumri na hata kwenye kazi hiyo ambayo mmoja wa walimu wangu wa chuoni Father Mfumbusa alikuwa akiidharau sana. ‘Kazi ya utangazaji redio ni ya ajabu sana, unajifungia kwenye kichumba unaongea peka yako,’ Mfumbusa alikuwa akisema mara kibao.
Ni kweli utangazaji ndivyo ulivyo lakini naapa nilipokuwa nikijifungua studio na kuanza kupiga mayowe peke yangu, nilijihisi kama dunia yote ni yangu. Niliipenda kazi ile na kwa wanaokumbuka masikio yao hayakuwadanganya jinsi nilivyosikika nikifurahia.
Mwaka 2007/08 Noorah alikuja Mwanza na hicho kilikuwa ni kipindi ambacho ukiambiwa umtaje rapper mwenye swagga na style kali za kuchana, ulikuwa huachi kumtaja Ngwair na Noorah. Si ajabu hasa ukizingatia kuwa wote walikuwa members wa Chamber Squad aka East Zoo.
Hivyo nakumbuka rafiki yangu Kidboy alimpeleka Noorah kwake kulipokuwa na studio za Tetemesha maeneo ya Kilimahewa. Kwenye gari ndogo tuliyokuwa tumepanda, kulikuwa kunachezwa wimbo wa msanii wa Canada mwenye asili ya Lebanon aliyetamba enzi hizo, Massari na wimbo wake Real Love. Noorah alikuwa akiuimba wimbo huo kwa kila mstari kama wake vile na kukibaini kipaji chake kingine cha kuimba.
Kwangu mimi na uanagenzi niliokuwa nao ilikuwa ni siku ya dhahabu kupanda gari moja na rapper huyo wa Shy town aliyekuwa si wa kukutana naye hivi hivi miaka ile. Noorah alikuwa wa moto na hakuna rapper aliyekuwa na uandishi na style kama yake. Hilo lilimpelekea kujibatiza jina na Babastylez.
Pamoja na kuanza kupata jina kupitia wimbo wake Vijimambo, umaarufu wa Noorah ulifika kileleni kupitia wimbo Ice Cream aliomshirikisha Sumalee na kutayarishwa na marehemu Roy kupitia G Records.

No comments:
Post a Comment