Juzi askari wa jeshi hilo, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walishinda mbele ya geti la nyumba ya askofu huyo kwa zaidi ya muda huo bila kufunguliwa na kuondoka bila kumkamata, hiyo ikiwa ni mara ya pili kwa chombo hicho cha dola kufanya hivyo katika kipindi cha miezi 16.
Baada ya kushindwa kumtia nguvuni mapema mwaka jana, Askofu Gwajima alijisalimisha kituoni siku iliyofuata.
Lakini jana, Gwajima hakufanya hivyo, na haijulikani alipo. Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema wanaendelea kumtafuta askofu huyo na kuwataka wenye taarifa za mahali aliko, waisaidie polisi.
Akieleza sababu za kwenda nyumbani kwake bila ya kumtaarifu askofu huyo, Kamanda Sirro alisema hawalazimiki.
“Si lazima apelekewe taarifa, askari walikwenda kwa nia njema ya kuonana naye ndiyo maana hawakutoa taarifa,” alisema Sirro na kuongeza: “Kama amejificha, tukimbaini alipo tutamkamata na atambue bado tunamtafuta.”
Askofu Gwajima anatafutwa na polisi katika kipindi ambacho mkanda unaodhaniwa una sauti yake, umezagaa kwenye mitandao ya jamii.
Sauti kwenye mkanda huo inasema Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo rais wa sasa, John Magufuli anayashughulikia.
Pia, sauti hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Magufuli asipewe uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu wa chama hicho.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa kile walichodai si wasemaji wa familia wala kanisa, watu wa karibu na askofu huyo walisema wanashangaa kuona polisi wanamtafuta bila kufuata taratibu kama kumuandikia barua.
Mmoja wa watu hao alisema hadi sasa wanashindwa kufahamu kama waliokuja kwa askofu ni askari kama inavyoelezwa au majambazi kwa sababu hawakuwa na sare wala vitambulisho.
Alisema sababu anayotafutiwa Gwajima ni kukinanga chama, wanaomtafuta ni wana usalama ambao hawatakiwi kuwa na chama kitu ambacho kinatia shaka.
No comments:
Post a Comment