Mbunge wa jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), jana alitema cheche Bungeni akimnyooshea kidole kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Lusinde alisema kuwa amepokea malalamiko kutoka kwa wabunge wa Chadema, wakitaka amfikishie taarifa Mwenyekiti wao huyo kwani hawawezi kumwambia.
Alisema wabunge hao wamemwambia kuwa wao hawapendi kususia vikao lakini wamekuwa wakilazimishwa na Mbowe.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya viongozi madikteta ndani ya nchi hii ni Mbowe [Freeman], anawatoa wabunge kwa nguvu. Wabunge [wa Chadema]wako hapo kwenye chai wamenituma mimi nije niwasemee humu ndani,” alisema Lusinde.
“Wameniomba, wamesema… ‘Lusinde kuna mambo sisi hatuwezi kumwambia Mbowe nenda ukamwambie’. Tunatumia fursa hii kumwambia Mbowe warudishe wabunge ndani ya Bunge, usiwanyanyase. Anawapigia simu wakae kwenye chai badala ya kuingia Bungeni, tabia gani hiyo,” alisisitiza.
Hata hivyo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi alikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa wabunge hao wanaamini kuwa hivi sasa wanaweza kuwawakilisha wananchi hata wakiwa nje ya Bunge na kwamba hivi sasa wanaendelea kufanya vikao vyao wakiijadili bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2016/17.
Sugu alisema kuwa wanaendelea kujadili Bajeti hiyo katika ukumbi wa zamani wa Pius Msekwa katika eneo hilo la Bunge na kwamba wanajadili pia njia bora zaidi ya kuwafikishia wananchi.
Akitolea ufafanuzi maelezo ya Lusinde, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Ackson Tulia alieleza kuwa wabunge wote wa upinzani wanaotoka Bungeni wakati vikao vya Bunge vikiendelea wanatoka kwa utashi wao na hawalazimishwi kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment