JUNI 20, 2016
DODOMA
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano kuhusu Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2015 na Mpango wa Maendeleo wa 2016/17 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2016/17, niliyowasilisha tarehe 8 Juni, 2016.
2. Mheshimiwa Spika, Kipekee, ninampongeza sana Mhe. Naibu Spika kwa umahiri na weledi wa hali ya juu alioonesha katika kusimamia Kanuni za Bunge wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la bajeti. Hakika viwango vyake ni vya kimataifa. Japokuwa Mhe. Joseph Kakunda, mwanafunzi wangu Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri, (nadhani alimaanisha bahiri wa kutoa maksi za upendeleo!), nataka niliambie Bunge lako tukufu kwamba kwa viwango ambavyo Mhe. Naibu Spika alivyoonesha humu ndani, hakika ningempa maksi za haki asilimia 100 kama walivyofanya maprofesa wake wa sheria UD na UCT. Hongera sana.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa na: Kamati ya Bajeti, chini ya M/kiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango, na waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni. Ninawashukuru wote.
4. Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 158 wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 133 wamechangia kwa kuzungumza na 25 kwa maandishi.
B: HATUA ZILIZOPONGEZWA NA WABUNGE WENGI
5. Mheshimiwa Spika, Hatua zilizopongezwa na Wabunge wengi wakati wa mjadala juu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2016/17 ni pamoja na zifuatazo:
· Kuthubutu kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja na kuanza ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge, barabara, umeme, ununuzi wa meli mpya ziwa Victoria na ndege tatu za abiria;
· Kuongeza ukusanyaji wa kodi na mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia wastani wa shilingi 1.2 trilioni kwa mwezi kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha matumizi ya vifaa vya kielektroniki (EFDs) katika ukusanyaji wa mapato, na Hazina kutoa fedha hizo kama ilivyopangwa;
· Kusimamia nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiwa pamoja na safari za nje, posho, sherehe, kuondoa watumishi hewa katika utumishi wa umma;
· Kuhimiza azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya watumishi kazini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa;
· Kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa PAYE na SDL kwa waajiri;
· Kuanzisha mahakama ya kushughulikia mafisadi;
· Kuweka kipaumbele katika kufufua na kujenga viwanda ili kupanua fursa za ajira na wigo wa kodi; na
· Kujielekeza kutekeleza Ilani ya CCM 2015, ahadi za viongozi wakuu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kutatua kero za wananchi, hasa masikini.
No comments:
Post a Comment