Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema wakati wa mchakato wa chama kurejesha imani kwa wananchi hali ilikuwa ngumu kwake hadi kufikia kutishiwa maisha na watu wasiojulikana.
Mbali ya watu hao kumpigia simu za vitisho nyakati za usiku, pia walikuwa wakimchafua kupitia mitandao ya kijamii lakini anamshukuru Mwenyezi Mungu alivuka salama na chama kimevuka salama.
“Tulipoanza kuzunguka kujenga chama nilitukanwa sana. Watu waliwekeza kunichafua. Watu hao niliokuwa nawanyooshea kidole hawakufurahishwa na hatua ile hivyo wakaweka mkakati wa kutaka kunifukuzisha ndani ya chama na ilifika hatua wakawa wananichafua katika mitandao ya kijamii.
"Nikaamua kujitoa huko mpaka leo hii nimeamua kujitoa katika mitandao na kubaki katika twitter pekee kwa kuwa unaweza kutambua mtumiaji,”alisema Nape.
Akizungumza nyumbani kwake mkoani Dodoma, Nape ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi na ambaye aliteuliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi hiyo mwaka 2011 Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete alipounda sekretarieti mpya chini ya Katibu Mkuu, William Mukama alisema watu hao walifikia kudai yeye si mtoto wa Mzee Moses Nnauye.
Kamati Kuu chini ya Mukama ilipita mikoani na kaulimbiu ya kuvua gamba iliyoasisiwa na chama kwa lengo la kuwaondoa watuhumiwa ufisadi lakini iliondolewa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2012 ikaundwa mpya chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Kukata vigogo
Katibu huyo wa uenezi alisema changamoto kubwa waliyokutana nayo katika mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM ilikuwa kukata majina ya waliokuwa viongozi wa Serikali ambao walijitokeza kugombea nafasi hiyo.
Katibu huyo wa uenezi alisema changamoto kubwa waliyokutana nayo katika mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM ilikuwa kukata majina ya waliokuwa viongozi wa Serikali ambao walijitokeza kugombea nafasi hiyo.
Nape alisema kumpata mgombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho kongwe ilikuwa kazi nzito baada ya viongozi mbalimbali wa juu wa Serikali ya Awamu ya Nne kujitokeza wakiwamo, aliyekuwa Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda na aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani.
Vigogo wengine waliowapa wakati mgumu CCM ni aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, na mawaziri kadhaa lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu waliweza kutimiza wajibu wao.
“Kuwaondoa viongozi waliokuwa madarakani ni sawa na kutafuna jongoo kwa meno lakini hatukutetereka na hatimaye tukapata majina matano ambayo nayo yalipigiwa kura na kupatikana jina la mgombea mmoja,” alisema.
“Ingawa vikao vilikuwa vya moto sana na kulazimika kukesha mpaka usiku, kila mmoja alipata nafasi ya kujadiliwa na kutendewa haki siyo kama ilivyovumishwa kuwa wagombea wengine hawakujadiliwa,”alisema.
Nape alisema katika chama chao kila mwanachama ana nafasi sawa hivyo haikuwasumbua kuangalia majina ya watu hao wala nyadhifa zao badala yake waliangalia sifa za mgombea mwenyewe ndani ya chama.
Alisema anashukuru Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Jakaya Kikwete kwa kuwa na kifua cha kuhimili vishindo na hiyo ndiyo siri ya kufanikisha mchakato huo kwa kuwa ni mtoto wa CCM hivyo ilikuwa rahisi kumkata yeyote kwani uzoefu wake ndani ya chama ulisaidia.
Nape alisema itachukua muda mrefu kupata kiongozi kama yeye lakini pia hawawezi kupuuza kazi iliyofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana na wazee waliorekebisha mambo na kuvuka salama kwa kuwa hali ilikuwa mbaya.
Bunge laivu
Nape alisema suala la kuzuia kurushwa moja kwa moja kwa matangazo ya Bunge si lake na kwamba lilipitishwa na wabunge wenyewe.
Nape alisema suala la kuzuia kurushwa moja kwa moja kwa matangazo ya Bunge si lake na kwamba lilipitishwa na wabunge wenyewe.
“Mimi ni msimamizi wa Serikali. Watu wanapotosha, nilichofanya ni kulinusuru Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), kwa miaka 10 mfululizo Bunge lilishindwa kuwalipa fedha zao ambazo ni Sh4.5 bilioni kila mwaka.
“Hili liwe fundisho kwa wabunge, kuna vitu wabunge wanapitisha hawavijui baada ya muda wanaona madhara yake wanaanza kulalamika kumbe walivipitisha wenyewe...Suala la Bunge kuanzisha kituo cha televisheni pia walilipitisha wenyewe, leo hii Katibu wa Bunge anavyotumia fedha kama ingekuwa haipo katika bajeti wasingemwacha,” alisema.
No comments:
Post a Comment