Licha ya uongozi wa Chadema
kutangaza kwamba umefuta mpango wa vijana wake (Bavicha), wa kuisaidia polisi
kuzuia mkutano mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki ijayo, jeshi
hilo limeimarisha ulinzi kila kona ya mji.
Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika
Julai 23, utashuhudia Rais John Magufuli akipokea kijiti cha uenyekiti wa chama
hicho kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Kikwete.
Kabla ya zuio la Mbowe, Bavicha
walikuwa wameanza kujiandikisha katika maeneo mbalimbali na kuchangisha fedha
kupata nauli ya kuja mjini Dodoma kuzuia mkutano huo huku polisi ikitangaza
kupambana nao.
Jana, polisi walifanya doria mji
mzima wa Dodoma na kisha kukutana na wamiliki wa nyumba za wageni na kuwataka
wageni wote watakaofika kwenye nyumba hizo kusajiliwa kwa vitambulisho
vyao.
Tukio hilo limekuja siku chache
baada ya kukamatwa kwa viongozi wa Bavicha ambao jana walifikishwa mbele ya
Hakimu Mkazi Dodoma kusomewa mashtaka na baadaye kuachiwa kwa dhamana wakidaiwa
kukutwa na maandishi ya uchochezi kinyume na kifungu cha 32 (2) cha Sheria ya
Magazeti, sura namba 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Waliofikishwa mahakamani ni
Mwenyekiti wa Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Julius Mwita, Mwenyekiti wa
Mkoa wa Mbeya, George Tito na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Joseph
Kasambala.
Akisoma mashtaka yao mbele ya
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Lina
Magoma alidai kuwa washtakiwa watatu; Katambi, Mwita na Tito walikutwa katika
Baa ya Capetown mjini hapa Julai 8 wakiwa na fulana zilizoandikwa lugha ya
uchochezi.
Alinukuu maneno yaliyoandikwa
katika fulana hizo kuwa ni “Mwalimu Nyerere: Demokrasia inanyongwa na Dikteta
Uchwara.”
Alisema upelelezi unaendelea na
kwamba hakuwa na pingamizi na dhamana. Kasambala alifunguliwa jalada lake pekee
licha ya shtaka lake kufanana na wenzake, tofauti ikiwa mahali alipokamatiwa na
ujumbe huo kwenye fulana aliyokuwa ameivaa.
Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana,
Kasambala alisema mshtakiwa huyo alikutwa katika Kituo cha Polisi cha Kati
Julai 9 akiwa amevaa fulana yenye maandishi; “Mwalimu Nyerere: Demokrasia
inanyongwa.” Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na Hakimu Mfawidhi Karayemaha,
aliwapa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo itatajwa tena Julai 26
mahakamani hapo.
Nje ya Mahakama
Akizungumza na wanahabari nje ya
mahakama hiyo, Katambi alisema tangu walipokamatwa Ijumaa iliyopita hawajawahi
kuambiwa kosa lao.
“Tulipokuwa Capetown tulipokwenda
kula chakula walitokea askari waliovalia kiraia na kutuvuta nje wakituambia
mkuu wao anahitaji kuzungumza na sisi lakini cha ajabu
hawakutuambia kosa kwa muda wote tuliokaa ndani,” alisema.
Alidai kuwa walihamishiwa katika
rumande nyingine zilizopo Chamwino kutoka Kituo Kikuu cha Polisi bila kuwaambia
ndugu, viongozi wa chama chao wala mawakili wanaowatetea.
Alisema katika rumande hizo kila
mshtakiwa alifungwa kwenye chumba chake. “... Sisi si majambazi lakini
polisi wametumia nguvu kubwa kutukamata na kutushikilia bila sababu ya msingi.
Lakini tuna imani Mahakama itatenda haki katika shauri hili.”
Kuimarisha ulinzi
Jana asubuhi, polisi waliokuwa wamebeba
silaha za moto, mabomu ya machozi na mbwa walionekana wakizunguka kwa pikipiki
na magari katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma.
Msafara wa magari zaidi ya 20
likiwamo basi kubwa lililobeba askari na gari la maji ya kuwasha, lilizunguka
katika mitaa mbalimbali kwa muda wa zaidi ya saa mbili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,
Lazaro Mambosasa alisema mara nyingi wamekuwa wakifanya mazoezi ya kutembea kwa
miguu lakini wakati fulani huwa wanatumia vyombo ambavyo wamepewa na Serikali
kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.
“Leo tumetoka kistaili ambayo
pengine haijazoeleka. Hatukuwa na matembezi ya miguu, tumetumia vyombo kwa
maana ya pikipiki na magari yote tuliyonayo. Haya ni mazoezi ya kawaida mara
nyingi tunafanya doria,” alisema.
Alisema doria hizo ni za pikipiki,
miguu na magari na kwamba yote yaliyoonekana jana ni katika kuwajenga askari
kuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na lolote litakalojitokeza akisema hayo ni
mazoezi ya kawaida na kwamba waliojitokeza ni maofisa wa polisi, wakaguzi,
askari wa vyeo vya juu na vya chini.
Alisema aghalabu wanafanya mazoezi
hayo usiku lakini kwa jana waliona wayafanye asubuhi ili kuwawezesha wakazi wa
Dodoma kujivunia chombo chao cha polisi.
Alipoulizwa kuhusu kauli za mitaani
kuwa mazoezi hayo ni ishara kuwa wanaogopa vijana wa Chadema, Mambosasa alisema
polisi hawaogopi mtu yeyote.
“Kwanza ijulikane tunafanya kazi
kwa mujibu wa Katiba ya nchi, sheria, kanuni, mwongozo na taratibu zote
zinazoongoza nchi. Kwa hiyo tunachokifanya si mambo mapya ni yale yaliyopo
kisheria,” alisema.
Alisema polisi hawaogopi wahalifu
wa aina yoyote hata wa kutumia silaha na wamejipanga kukabiliana nao.
“Na niwaambie tu... haogopwi mtu
hapa, sisi tunasimamia sheria kwa kuwaelimisha watii sheria bila shuruti na
wale wachache wasiotii tutawashurutisha,” alisema.
Alisema wale wote wanaosema
watafika Dodoma kulisaidia jeshi la polisi watawashurutisha kwa kutumia nguvu
kidogo tu ili warudi kwenye mstari.

No comments:
Post a Comment