Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
imeyatupilia mbali maombi ya kuzikwa Tanga mwili wa Andrew Daffa, aliyefariki
dunia Jumatano iliyopita katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.
Mwili wa Daffa ulizuiwa kuzikwa
kutokana na maombi ya kesi ya madai namba 240 ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na
baba yake, Charles Joseph ambaye alitaka apewe kibali cha kumzika mwanaye
Kijiji cha Vigiri mkoani Tanga alikozaliwa.
Mvutano huo ulijitokeza baada ya
mke wa marehemu, Glory Charles kutaka kupewa haki ya kuzika mwili wa mumewe
katika makaburi ya Kwa Jimmy yaliyopo Yombo Vituka.
Glory aliieleza Mahakama kuwa eneo
hilo ndilo walilozika watoto wao watano, ambao alizaa na mumewe.
“Kwa sababu mume wangu alikuwa
anaishi na mimi Tabata Kimanga na nilimuuguza mpaka dakika ya mwisho bila
kupata msaada wa ndugu yeyote, naomba Mahakama inipe kibali cha kumzika kwani
na mimi nina haki kama mke,” alidai Glory,
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Adelf Sachore alisema Mahakama inatupilia mbali
maombi ya baba wa marehemu, hivyo inaamuru mwili huo apewe mke wake.
“Maombi ya baba wa marehemu
yanatupiliwa mbali, Mahakama inaamua mwili huo uzikwe walikozikwa watoto wake
waliofariki dunia,”alisema.
Hakimu Sachore alisema katika kesi
hiyo, Wakili wa utetezi, Daniel Buma alidai marehemu anatakiwa azikwe mkoani
Tanga kwa madai kuwa ndiyo mila zao zinavyoeleza kwa sababu hana makazi ya
kudumu Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mahakama ilipokea
vielelezo kutoka kwa mlalamikiwa (Glory) ambavyo ni cheti cha ndoa na picha za
watoto wao waliokufa na vyeti vya watoto waliopo.
Baada ya kutolewa uamuzi huo, Glory
alibubujikwa machozi ya furaha na kuomba Mahakama impe ulinzi wakati wa mazishi
ya mumewe yanayotarajia kufanyika leo katika makaburi ya Yombo Vituka.

No comments:
Post a Comment