CHAMA cha Wananchi (CUF) kimelitaka
Jeshi la Polisi kuwapandisha mahakamani viongozi wake wanaowashikilia kwa
tuhuma za uchochezi kisiwani Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari
visiwani hapa jana, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho,
Salim Bimani, alisema kama polisi wana ushahidi wa viongozi wa CUF na wafuasi
wao kujihusisha na matukio ya uvunjifu wa amani basi wawapeleke mahakamani.
Bimani alisema wanasikitishwa na
hatua ya jeshi hilo kuwaweka ndani viongozi na wafuasi wao kwa muda mrefu bila
ya kuwafikisha mahakamani kinyume na haki za binaadamu.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kama
wana ushahidi juu ya viongozi wetu ambao wanawahusisha na matukio ya uvunjifu
wa amani kisiwani Pemba basi wawapeleke mahakamani,” alisema
Bimani.
Bimani alisema kuwa tokea
kuanzishwa mfumo wa vyama vingi Tanzania kumekuwa na unyanyasaji na
udhalilishaji dhidi ya raia hasa wanachama wa CUF jambo ambalo alisema kuwa
linafanyika kwa nia ya kukikandamiza chama hicho.
“Ikiwa sehemu ya utekelezaji wa
mkakati huo kila wakati Zanzibar imekuwa ikishuhudia kuletwa askari wengi
katika kipindi cha uchaguzi,”alisema Bimani.
Hata hivyo, alisema kuwa baada ya
kumalizika kwa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, kumekuwa na hatua kadhaa za
unyanyasaji dhidi ya wafuasi wa chama hicho unaofanywa na vyombo vya ulinzi na
usalama.
“Haya yote yanayofanyika ili kuzima
sauti za watu, lakini tunawaambia viongozi wa CCM pamoja na vyombo vya dola,
tutaendeleza msimamo wetu wa haki sawa kwa wote,” alisema Bimani.
Alisema CUF inalaani vitendo vya
hujuma dhidi ya raia na mali zao unaofanywa kwa lengo la kuvipa sababu vyombo
vya ulinzi na hasa wafuasi wake, pamoja na kulaani kauli za vitisho na lugha za
kibabe zinazotolewa na Jeshi la Polisi Zanzibar, kama vile iliyotolewa Juni 28
mwaka huu na Naibu Mkurugenzi wa Upepelezi Salum Msangi kisiwani Pemba kwa
lengo la kuwanyamazisha wananchi ili kuisambaratisha CUF.

No comments:
Post a Comment