
TAASISI ya Maridhiano inatarajia
kuwasilisha ujumbe kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kuomba kuyakutanisha makundi
mawili yanayosigana bungeni ili kuleta muafaka wenye tija kwa taifa.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sheikh
Sadick Godigodi jana alisema kumeguka kwa Bunge kunakosababishwa na Kambi ya
Upinzani kuona inaonewa na maamuzi ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson kunahitaji
viongozi wa dini kuingilia kati na kupata suluhu.
"Tunatarajia katika Bunge
lijalo litakaloanza Septemba kuwasilisha ujumbe kwa Spika ili tupewe nafasi ya
kutatua mgogoro huu kwa maana wabunge wote wanatakiwa kuwepo bungeni
kuwakilisha matatizo ya wananchi," alisema Sheikh Godigodi.
"Haiwezekani kundi moja likawa
nje na jingine likaendelea, tunahitaji maridhiano ya pande zote mbili za
muhimili huo.”
Kambi ya Upinzani Bungeni ilisusia
vikao vya Bunge la Bajeti kwa zaidi ya siku 70 kupinga kile kilichoita
kuburuzwa na
Naibu Spika katika uendeshaji wa
chombo hicho cha kutunga sheria.
Kambi hiyo, ilianza kutoka nje Mei
30 baada ya Naibu Sika kukataa hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari (Chadema), ya kutaka Bunge
likatize shughuli zake na kujadili hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi zaidi ya 700
wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Ingawa kitendo hicho cha Naibu
Spika kiliwaudhi wabunge wa chama tawala (CCM) na Upinzani, kambi hiyo
haikurudi ndani mpaka Bunge lilipoahirishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
katikati ya wiki iliyopita.
Mshauri wa mambo ya kisheria na
kidiplomasia wa taasisi hiyo ya Maridhiano, Agustino Matefu alisema mbali na
kusuluhisha migogoro chochezi ya kidini kwa kutoa elimu sahihi kwa umma, pia
wamejikita katika kusuluhisha migogoro sugu kati ya wakulima na wafugaji
nchini.
“Tumetoa mchango mkubwa wa kuleta
suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima mkoani Morogoro
katika wilaya za Mvomero, Kilombero na Kilosa (na) ndio maana watanzania
wanaona hali ni kama sasa imekuwa shwari,” alisema Matefu.
Matefu alisema wamepata mualiko
rasmi kwa uongozi wa Mkoa wa Iringa na wanatarajia kwenda huko baada ya
uzinduzi rasmi wa taasisi hiyo utakaofanyika Julai 13 jijini Dar es Salaam.
Katibu wa taasisi hiyo, Mchungaji
Oswald Mlay alisema kuwa uzinduzi na utambulisho wa taasisi hiyo utaendana na
utoaji tuzo ya amani kwa viongozi na watu mbalimbali waliojitoa kuhamasisha
udumishwaji wa amani nchini.
Wanaotarajiwa kupewa tuzo ni Mama
Maria Nyerere kwa niaba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambae atatunukiwa
tuzo ya Amani uasisi wa amani ya taifa.

No comments:
Post a Comment