
KAMPUNI ya Usafirishaji ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es
Salaam (UDART) inatarajia kusitisha matumizi ya tiketi za karatasi ifikapo
Julai 30 mwaka huu.
Uamuzi huo unalenga kudhibiti foleni za kununua tiketi za
karatasi kutokana na idadi kubwa ya abiria; kati ya 150,000 na 200,000
wanaotumia usafiri wa mabasi hayo kwa siku.
“Kwa siku abiria wapatao laki moja na nusu hadi laki mbili
wanatumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka kila siku, sasa kumekuwa na foleni
vituoni na pia tunakusanya magunia na magunia ya karatasi na kuna maeneo
mengine uchafu unakuwa mwingi,” Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa aliwaambia waandishi
wa habari jana.
Hata hivyo, kusitishwa huko kwa tiketi za karatasi, kunalenga
watu wazima pekee wanaolipa Sh 650. Wanafunzi wanaolipa Sh 200, wataendelea
kutumia tiketi za karatasi ambazo zitakuwa zikipatikana kwenye vituo vya
mabasi.
Mgwasa alisema licha ya hatua hiyo kulenga kupunguza foleni
kwenye vituo, pia itaondoa uchafu unaotokana na tiketi za karatasi.
Wakati huo huo, alisema kutokana na mpango huo wa kusitisha
tiketi, kuanzia leo kampuni imepunguza gharama ya ununuzi kutoka Sh 5,000 kwa
tiketi za hadi Sh 2,000, Sh 500 itakuwa gharama ya kadi na Sh 1,500 ni nauli.
“Kuanzia kesho (leo) kadi zitauzwa kwa gharama ya Sh 2,000
kwenye vituo vyote vya mabasi ya mwendokasi,” alisema.
Mgwasa alisema tangu kuanza kuuzwa kwa kadi hizo kwa gharama ya
Sh 5,000 tayari kadi 55,000 zimeshanunuliwa na kubakia kadi 150,000 ambazo ziko
kwenye promosheni ya kuuza kadi kwa Sh 5000.
Alisema baada ya kadi hizo kuisha, abiria atalazimika kununua
kadi hiyo kwa thamani ya Sh 5,000 bila kuwekewa fedha za nauli kama ilivyokuwa
awali.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Maxcom Afrika (MaxMalipo),
Deogratius Lazari alisema wamejipanga kuhakikisha tiketi za kadi zinapatikana
kwenye vituo vya mabasi. Aliwataka wateja kuhakikisha wanaweka salio katika
vituo hivyo.
“ Kampuni za simu ziko katika hatua ya mwisho za kukamilisha
mifumo yao ili abiria aweze kuongeza salio kupitia mitandao ya simu ila kwa
sasa abiria wanatakiwa kutumia vituo vyetu vya mabasi na wakala wa max malipo,” alisema.
Mabasi ya haraka yalianza kutoa huduma Mei mwaka huu kwa kuanza
na tiketi za karatasi na baadaye, kuanzishwa utaratibu wa kadi ambao
haujaitikiwa kwa kiwango kikubwa.

No comments:
Post a Comment