
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno endapo Rais John Magufuli atamhitaji
kuendelea na wadhifa huo, huku akibainisha kuwa amekutana na changamoto nyingi
katika nafasi hiyo kiasi kwamba wakati mwingine alikata tamaa.
Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jeshi.
Akizungumza jana na waandishi wa
habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu wa CCM utakaofanyika
keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu
na nusu, alisema aliombwa katika nafasi hiyo baada ya kuwa aliamua kustaafu,
lakini akakumbana na changamoto mbalimbali.
CCM kuwa mbali na wananchi
Alisema kuna wakati aliona kama
vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba hakikuwa karibu sana nao.
“Ninyi ni mashahidi, ikabidi kubuni
utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili chama kiwe karibu na wananchi,
kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi kifuatilie matatizo yao kisimamie
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,” alisema Kinana na kuongeza
kuwa katika kufanya hivyo amekuwa akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili
ya matatizo kutatuliwa.
“Changamoto ya pili ya kuimarisha
umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma kulikuwa na misukosuko kidogo ya
umoja na mshikamano, kushutumiana na kulaumiana,” alisema na
kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni kuimarisha umoja ndani ya chama,
kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha chama kinajitahidi kwa kadri ya
uwezo wake kurejea katika misingi yake ya awali katika maeneo ya uadilifu,
uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi.
Azuiwa ziarani
Kinana alisema amekwenda wilaya
zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi na amesafiri zaidi ya kilometa
192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700 ya aina mbalimbali ya ndani na nje na
haikuwa kazi rahisi
“Changamoto nilizokutana nazo
ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati mwingine kufanya ziara kwenye
maeneo fulani fulani niliambiwa ni hatarishi siwezi kwenda kwa hiyo ilibidi
nibishane na viongozi na watendaji wakuu wa serikali…nikasema hapana nimeamua
kwenda lazima niende,” alisema Kinana.
Katibu huyo akitoa mfano alisema
kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka Nyamisati wilayani Rufiji kwenda
Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani walifikiri si njia salama ya kusafiri na
kumpelekea ujumbe asisafiri kwa boti, bali asafiri kwa ndege, lakini alisema
hapana ataondoka kwa boti.
“Walichofanya wakakaa kikao cha
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia barua rasmi kwamba
tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa maana nyingine walikuwa
wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile vile kunitisha kidogo kwamba si
salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.
Ashitakiwa kwa JK
“Baadaye Rais mstaafu Kikwete
alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda kumwambia tumezungumza na
Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia barua ya kumuomba asisafiri na
boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu sana…nikamjibu rais nakuheshimu
mamlaka yako ni makubwa si vizuri nikakukatalia, lakini niruhusu nikukatalie
kwa sababu hata wananchi wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha maisha yao,
ni vizuri na mimi nikahatarisha maisha yangu hata kidogo… akaniambia
nimekuelewa endelea,” alibainisha.
Alisema zipo changamoto nyingi sana
nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela, mkuu wa mkoa akamuambia boti haifai
kusafiri akasema mara haiwezi kusafiri imeharibika.
“Nikazungumza na Mwakyembe
akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi, lakini changamoto
zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari moja tu ndio inayoshuka chini
hakuna kupishana magari nikaambiwa nisiende nikasema nina kwenda,” alisema na
kuongeza kuwa kulikuwa na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja
kidogo ambaye hasikilizi ushauri sana.
Pia nyingine zinazotokana na
changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa wakati, mbolea kutofika kwa
wakati, halmashauri kutopata fedha za maendeleo kwa wakati, watumishi wa umma
wanaohamishwa kwenda vijijini hawaendi vijijini kwenda kuwahudumia wananchi,
tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kati ya wananchi na
hifadhi za taifa.
“Ndio maana mnaniona siku hizi
nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa nikiyaombea yanafanyika, umangimeza
haupo watu wachape kazi wawahudumie wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa
inapigwa vita, uwajibikaji na uadilifu unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na
hayo yasipofanyika mtu anaondolewa mara moja,” alifafanua Kinana ambaye kuanzia
mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha
chama chake na kuibana serikali.
Kurejea kwake CCM
“Yalitokea mazingira ambayo
niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama kuniomba niwe mtendaji mkuu
wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda, bali niliitwa na nikakalishwa
wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni wito na kwa kuwa ni watu ninaowaheshimu
na wana dhamana kubwa kwenye nchi yetu, nikakubali kufanya kazi hiyo,” alisema Kinana
akizungumzia jinsi alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Alisema amekuwepo katika uongozi
ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu
ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka wa kung’atuka.
“Mwanasiasa mzuri ni yule anayejua
wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati mzuri wa kung’atuka kuachia
waingie wenye umri wa kati na umri wa vijana kuachia waongoze chama na kuwaamini,”alieleza.
Alisema moja ya mambo ambayo
walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha chama, kusimamia na kumsaidia
mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata wagombea kwenye nafasi zote za Urais,
Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi kuendesha shughuli za kampeni na uchaguzi na
utakamalizika.
“Uchaguzi umekwisha niruhusiwe
kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda umefika kwa hiyo
nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika sasa wengine wakaniuliza
hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee hamjawa wazee kiasi cha kusahau
ndio haya tuliyokubaliana,” alieleza.
Akiombwa na JPM
Alipoulizwa kama akiombwa na Rais
Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme hajasema,
hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye kikao kama akiniomba,
tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika kama nilivyokuwa na mazungumzo
na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka 2012.”
Waliokisaliti chama
Akizungumzia walioisaliti CCM
katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM alisema msaliti yeyote
adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha siasa.
“Kwenye CCM wapo watu walioyumba,
kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu waliyumba hivi kidogo wakakaa mguu
upande huku hawapo na kule hawapo, wako ambao sio tu waliyumba, bali walikiuka
maadili na hawakushiriki kwenye shughuli za kampeni,” alisema.
Pia alisema wapo ambao
hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani na kila mtu atakuwa na
adhabu yake kulingana na makosa yake.
“Kama mmekuwa mkifuatilia kuna
waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa. Kwa mfano, Shinyanga 123
walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kwenye ngazi za juu,
sasa jambo moja mtu yeyote kabla ya kuchukuliwa hatua lazima aelezwe mashtaka
yake, apewe fursa ya kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote watasomewa mashtaka, watasikiliza
na kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili, lakini hatua zitachukuliwa mara
baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,”alieleza.

No comments:
Post a Comment