
Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi
ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ana uhakika kuwa bado kuna wanachama
wanaomuunga mkono ndani ya CCM na sasa anawataka waendelee kushikamana naye,
kauli ambayo inaweza kuchochea moto ndani ya CCM.
Katika taarifa yake fupi kwa vyombo
vya habari aliyoitoa jana, Lowassa amewahakikishia wananchi kuwa kwa sasa ana
“ari, nguvu na hamasa kuliko wakati mwingine wowote”.
Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu
wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alijiondoa kwenye chama tawala Julai 28
mwaka jana baada ya jina lake kuondolewa kwenye orodha ya wagombea urais kwa
tiketi ya CCM.
Kuondoka kwake kulisababisha
mawaziri wa zamani, wabunge, wenyeviti wa mikoa, madiwani na wanachama wengine
wa CCM, wakiongozwa na waziri mwingine mkuu wa zamani, Frederick Sumaye
kukihama chama hicho, hali iliyosababisha ushindani kuwa mkubwa kwenye Uchaguzi
Mkuu uliopita, huku CCM ikilalamikia kusalitiwa.
Wakati CCM ikifikiria hatua za
kuchukua dhidi ya wasaliti wa chama wanaotuhumiwa kuunga mkono harakati za
upinzani wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Lowassa ameongeza petroli kwenye
moto ulioanza kuwaka.
“Kwa wale wenzangu waliobaki CCM na
wanaoniunga mkono, tuendelee kushikamana na kunipatia taarifa kwa hatima ya
nchi yetu,”amesema Lowassa ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema.
“Nawashukuru Watanzania kwa
kuendelea kuniunga mkono mimi na wenzangu ndani Chadema.”
Kauli hiyo kuwa kuna watu ndani ya
CCM ambao wanampatia taarifa mbunge huyo wa zamani wa Monduli na ombi lake la
kutaka waendelee kumpa taarifa, inaweza kusababisha hali ngumu zaidi kwa chama
hicho, ambacho kinaamini kuwa makada wake walikihujumu wakati wa uchaguzi kwa
kumfanyia kampeni kisiri.
Katika uchaguzi huo, Rais John
Magufuli alishinda kwa kupata asilimia ndogo ya kura kulinganisha na
watangulizi wake.
Ingawa alipata kura milioni 8.8 na
Lowassa kufuatia kwa kupata kura milioni 6.07, ushindi huo ni wa asilimia 58.46
dhidi ya asilimia 39.67 kulinganisha na ushindi wa asilimia 61.17 aliopata
Kikwete mwaka 2010 dhidi ya asilimia 26.34 alizopata Dk Willibrod Slaa wa
Chadema.
Tangu Januari mwaka huu, CCM
imekuwa ikijadili wasaliti hao katika ngazi ya wilaya na taarifa za mapendekezo
ya hatua dhidi yao kutumwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Katika hotuba yake ya kuaga, Jakaya
Kikwete alimkabidhi mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Magufuli ripoti ya hali
ilivyokuwa kwenye uchaguzi, akisema yeye ndiye atakayeamua adhabu dhidi ya wale
wote walioonekana kufanya makosa. CCM imeshasema kuwa wasaliti wote ni lazima
washughulikiwe.
Katika taarifa yake ya jana,
Lowassa ameeleza kuwa uamuzi alioufanya wa kuihama CCM na kujiunga na Chadema “haukuwa
rahisi, lakini kwa ushupavu, ujasiri na mwongozo wa Mungu nilifanya hivyo” na
kwamba huo ni “uamuzi wa kihistoria katika nchi yetu.
“Najivunia kwa uamuzi ule, kwani
umewafungua macho Watanzania wengi na kuimarisha demokrasia. Nimeingia Chadema
nimewakuta viongozi na wanachama walio na moyo wa dhati wa kuliletea maendeleo
Taifa lao kivitendo,” anasema Lowassa katika taarifa yake fupi.
“Watanzania bado wanataka
mabadiliko na imezidi kuthibitisha kuwa hawawezi kuyapata ndani ya CCM.
Watanzania wanataka sera na mtu mbadala wa kuongoza mabadiliko hayo. Vyote
hivyo watavipata ndani ya Chadema na Ukawa kwa jumla.”

No comments:
Post a Comment