VITENDO vya ukatili wa kijinsia na
dhuluma dhidi ya watoto wa kike vimekuwa vikishamiri kila siku pamoja na kuwepo
kwa taasisi za kutetea haki za wanawake na kuanzishwa kwa madawati ya
Kijinsia kwenye vituo vya polisi nchini.
Msichana wa kidato cha Nne mwenye
umri wa miaka 17,(jina tunalo) anayesoma shule moja ya sekondari ya Kata mkoani
Mbeya amekumbwa na kadhia ya kuvuliwa nguo zake za ndani na kucharazwa
bakora zisizo na idadi na walimu wanne wa shule hiyo.
Tukio hilo ambalo limeripotiwa
katika kituo kidogo cha Polisi Mbalizi wilaya ya Mbeya kwenye jalada la
uchunguzi namba MBI/IR/967/2016na kuwekwa kwenye taarifa yenye
namba MBI/RB/2653/2016 linadaiwa kuwahusisha walimu wanne
akiwemo Mkuu wa shule hiyo pamoja na walimu watatu.
Akizungumza huku akiwa na maumivu
makali katika Hospitali Teule ya Ifisi ambako amelazwa akipatiwa matibabu,
mwanafunzi huyo alisema kuwa aliitwa na mwalimu wa nidhamu aliyemtaja kwa jina
la Neema Mwaikenda aliyekuwa pamoja na Mkuu wa shule hiyo aliyemtaja kwa jina
la Mariamu Mwanisenga na mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili.
Alisema walimu hao walianza
kumuadhibu kwa viboko visivyo na idadi huku akiwa amechojolewa nguo zake ambapo
mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili akaanza kumshikashika sehemu zake
za siri.
‘’Wakati naadhibiwa na walimu wote,
huyu mwalimu wa kiume alianza kunishika huku chini,na kunitaka niwataje
wanaume zangu,nikawa nabana miguu wakazidi kunishambulia kwa vibao na mateke na
fimbo,’’alisema mwanafunzi huyo.
Alisema sababu zilizosababisha
aadhibiwe ilikuwa ni utoro na kuwa siku moja alipokuwa shuleni alioneshwa na
walimu fimbo na kuelezwa kuwa fimbo hizo zitamuishia mwilini ndipo akaogopa
kufika shuleni kwa siku tatu.
Anafafanua kuwa siku aliyofika
shuleni ndipo alipokutana na kadhia ya kupigwa na walimu wanne hadi
alipowaponyoka walimu hao na kukimbilia mitaani na kujificha.
‘’Niliwaponyoka walimu nikakimbilia
kwenye nyumba ya jirani na shule nikajificha hadi jioni na baadaye kwenda
nyumbani, kesho yake mama na dada walinichukua na kunileta hospitali,’’alisema.
Mwandishi wa habari hizi alifika
shuleni anakosoma mwanafunzi huyo kwa nia ya kukutana na uongozi wa shuleni
hiyo ambapo Makamu Mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la
Mwansanga alikataa kuelezea chochote.
‘’Mie sijui lolote kwanza mie sio
msemaji wa shule, kwahiyo sijui lolote juu ya taarifa mnazohitaji,’’alijibu Makamu
Mkuu wa shule na kuondoka zake.
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa
Charles Mwakalila alisema kuwa adhabu aliyopewa mwanafunzi huyo ni kubwa
kupitiliza kwa kuwa zipo taratibu za adhabu kulingana na makosa na kuwa
mwanafunzi anapaswa kupigwa viboko vitatu na viboko visivyozidi sita au adhabu
mbadala.
‘’Adhabu aliyopewa ni kubwa,
tutafuatilia na waliokiuka taratibu watachukuliwa hatua za kinidhamu,’’alisema
Mwakalila.
Naye Kamanda wa Polisi wa mkoa wa
Mbeya Dhahiri Kidavashari alipoulizwa juu ya tukio hili alidai kuwa halijafika
ofisini kwake na kuwa kwa sasa yeye yupo kikazi wilayani Chunya na mara
atakapofika ofisini atafuatilia na kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika wa
tukio hilo.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa
Mbeya Mariamu Mtunguja ambaye alifika Hospitalini alikolazwa mwanafunzi huyo
alisema kuwa amemuangalia mwanafunzi huyo na kuona namna ambavyo damu imevilia
kwenye sehemu zake za makalio na kwenye mapaja.
Mtunguja alisema kuwa kitendo
kilichofanywa na walimu hao ni cha kinyama ambacho hakipaswi kuvumiliwa na kuwa
mara itakapobainika atahakikisha walimu hao wanachukuliwa hatua za kinidhamu.
Muuguzi Mkuu Msaidizi wa Hospitali
Teule ya Ifisi Elimati Sanga alisema kuwa mwanafunzi huyo alifikishwa
hospitalini hapo Julai 21 saa 7:00 mchana ambapo alipatiwa matibabu na kulazwa
kutokana na majeraha na damu iliyovilia mwilini sehemu za makalio na mapaja.
‘’Ameshambuliwa sehemu za mapaja,
damu na masikio yake hasikii vyema kutokana na kipigo, anaendelea na matitabu
hapa hospitali,’’alisema Sanga.
Muuguzi Mkuu msaidizi wa Hospitali Teule ya Ifisi, Elimati
Sanga akielezea madhara aliyopata mwanafunzi anayedaiwa kupigwa na walimu wanne
wa shule ya Sekondari Malama
No comments:
Post a Comment