Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi
(CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la Polisi kama lina nia ya
kumkamata na kumweka ndani lifanye hivyo kwa kuwa yeye yupo nchini.
Akizungumza katika Baraza la Eid el
Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Wakfii wa Ngazija mjini Zanzibar, tofauti
na jingine lililofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani na
kuhutubiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Maalim Seif alisema nchi
inapita katika kipindi kigumu kutokana na dhuluma inayotendwa na watawala dhidi
ya raia wasiokuwa na hatia.
“Huwezi kuamini kuwa dhuluma hii
inatendwa na watawala Waislamu. Hali ni mbaya, wananchi wanapata hilaki kubwa
baada ya hao wanaojiita Serikali kubaini kuwa hawakubaliki.
"Mambo hayo yanafanywa
kutokana na kushindwa kuzigeuza nyoyo za wananchi ndiyo maana wanafanya hujuma,
vitendo vya kikatili na kuwatisha wananchi,” alisema Maalim
Seif.
Maalim Seif alieleza kusikitishwa
na hali ya kamatakamata dhidi ya viongozi mbalimbali wa CUF katika ngazi za
wilaya na majimbo na kuwekwa ndani huku wakiteswa, kuadhibiwa na kulazimishwa
kukubali kushiriki katika vitendo vya uhalifu ambavyo hawakuvitenda.
Alibainisha kuwepo mwendelezo wa
kauli zinazoashiria azma ya kutaka kumkamata yeye, zinazotolewa na baadhi ya
wakuu wa vyombo vya dola.
“Hakuna haja ya kuwatesa watu,
iwapo wanayo azma ya kunikamata, mimi nipo waje tu wanikamate,” alisema
Maalim Seif.
Maalim Seif alisema vitendo vyote
hivyo ni mwendelezo wa dhuluma aliyoitenda Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha, tarehe 28 Oktoba 2015 wakati akifuta matokeo
ya Uchaguzi Mkuu kabla ya kuitisha ule wa marudio wa Machi 20.
Hii ni mara ya kwanza mpasuko wa
kisiasa unawaathiri Wazanzibari hata wakati wa Sikukuu ya Eid -El Fitr
inayoadhimishwa baada ya kumalizika mfungo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Akihutumia Baraza lililofanyika
katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Dk Shein aliendelea kukazia
kuwa Zanzibar haitakuwa na uchaguzi mwingine mpaka mwaka 2020 kwa kuwa Serikali
iliyochaguliwa na wananchi imeshaundwa.
Katika hotuba hiyo ya takriban
dakika 35, alisema hakutakuwa na Serikali ya mpito na kueleza kuwa hayo
“yanayosemwa mitaani ni maneno ya wababaishaji.”

No comments:
Post a Comment