
Mzazi aliyejifungua watoto watatu
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini akazuiwa wodini kutokana na
kudaiwa gharama za matibabu, jana aliruhusiwa kuondoka baada ya Waziri wa Afya,
Ummy Mwalimu kuingilia kati suala hilo.
Mzazi huyo, Stella Nnko (38)
aliyefikishwa Muhimbili kwa rufaa akitokea Hospitali ya Mnazi Mmoja, alikuwa
akidaiwa Sh540,595.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ndiye
aliyeingilia kati suala hilo na kuagiza mama huyo apewe watoto wake na
kuruhusiwa ambapo jana asubuhi katibu mkuu wa wizara, Dk Mpoki Ulisubisya
alimtembelea mzazi huyo kabla ya kuondoka hospitalini hapo.
Akizungumzia tukio hilo, Stella
alimshukuru Waziri kwa kuingilia kati suala hilo na kuwaomba wasamaria wema
kumsaidia katika matunzo ya watoto hao kwa kuwa uwezo wake kiuchumi si mzuri.
Alisema hajawahi kuonana na baba wa
watoto hao tangu alipompa ujauzito, na yeye hana uwezo wa kuwatunza.
“Ninayaendesha maisha yangu kwa
kukaanga mihogo, shughuli ambayo kwa sasa nitashindwa kuendelea kuifanya kwa
sababu ya kuwahudumia hawa watoto,” alisema Nnko.
“Nyumbani nimemwacha mwanangu wa
miaka miwili na nusu na sina msaidizi wala ndugu.”
Stella anaishi Kivule, Ilala jijini
Dar es Salaam. Kabla ya kuondoka Muhimbili, watoto hao watatu walipewa chanjo
ya kupooza, BCG ya kifua kikuu na matone ya vitamin A.
Mtoto mmoja kati yao ni wa kiume na
alizaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 2.8 wakati wa kike wawili walikuwa na
uzito wa kilo 2.5 na 2.1.
Akizungumzia sakata hilo, mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha MNH, Aminiel Aligaesha alisema Stella
alifikishwa hospitalini hapo Juni 29 mwaka huu kwa dharura akitokea Mnazi Mmoja
na kufanyiwa upasuaji Juni 30.
Lakini alikanusha taarifa kwamba MNH
ilimzuia kutoka, bali alipewa hati ya malipo ili ajiandae kulipa, kinyume na
kauli ya Stella kwamba aliruhusiwa kuondoka na kupewa hati ya malipo na
alipoeleza kuwa hana uwezo, alizuiwa mpaka atakapochangia huduma.
“Wakati Stella akipewa huduma na
kusubiri kuruhusiwa, alipelekewa gharama ya jumla ya Sh477,131 ikiwa ni gharama
ya kujifungua kwa upasuaji na huduma zote alizozipata tangu alipopokelewa,
zikiwemo dawa na vitendanishi. Hakuzuiwa, ila alipewa hati ya malipo ili
ajiandae kulipa,” alisema Aligaesha.
Alisema pamoja na hayo, Nnko
amesamahewa kulipa gharama zote za matibabu na tayari amesharuhusiwa kwenda
nyumbani.
Kuhusu suala la tozo kwa mama
wajawazito, Aligaesha alisema ni utaratibu ambao uliwekwa na hospitali wa
kuchangia huduma kwa kuwa tangu wameanza mfumo huo dawa na vitendanishi
vimekuwa haviadimiki ikilinganishwa na hapo awali.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha kila
mgonjwa anayekuja kutibiwa MNH anapata dawa na huduma zote kwa gharama nafuu.
Tunawaomba wananchi kuchangia huduma zote za afya ili tuweze kupata fedha na
kutoa huduma kwa mfumo endelevu.Ndiyo maana ndani kuna duka la MSD,” alisema
Alisema iwapo akitokea mgonjwa hana
uwezo wa kuchangia huduma, utaratibu wa kumuombea msamaha unatumika na atapata
huduma bila malipo.
Maiti iliyozuiliwa
MNH pia ilidaiwa kuzuia mwili wa
marehemu Hilda Mbawala aliyefariki Juni 26 kutokana na ndugu zake kushindwa
kulipia gharama za Sh1.4 milioni, lakini Aligaesha alikanusha madai hayo.
“Wakati marehemu akitibiwa, ndugu
walikuwa wanapewa taarifa na mwenendo wa matibabu ya ndugu yao, ikiwamo
kuhimizwa kuchangia huduma,” alisema Aligaesha.
“Baada ya kifo hicho, ndugu wa
marehemu walipewa hati ya gharama ya matibabu ya Sh1.4 milioni ili wakajipange
jinsi ya kulipa.”
Alisema ndugu hao walisema hawana
uwezo wa kulipia kiasi hicho cha fedha na Juni 30 waliwasiliana na Ofisi ya
Ustawi wa Jamii ili wasaidiwe na baada ya majadiliano pande zote mbili
zilikubaliana kuwa walipe Sh800,000.
“Wakati makubaliano hayo yakiwa
kwenye hatua za kuidhinishwa na mamlaka husika, ndipo ndugu walipokimbilia
kwenye vyombo vya habari na kulalamika kuwa hospitali imezuia mwili.
"Ukweli ni kwamba wamelipa
kiasi hicho cha Sh800,000 na wamesamehewa deni la Sh 623,747.64 na mwili
waliuchukua Julai 5,”alisema.

No comments:
Post a Comment