
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi
(GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’
amesema kitendo cha viongozi wa CCM kulitaja zaidi jina la Edward Lowassa
katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho ni ishara kuwa Waziri Mkuu huyo wa
zamani ni tishio.
“Nani! Lowassa…. jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio. Ndiyo ni tishio,” alisema Lusekelo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Lusekelo ambaye hivi karibuni, Rais
John Magufuli alishiriki ibada katika kanisa lake, alimzungumzia Lowassa baada
ya kuulizwa swali juu ya mtazamo wake kuhusu Mkutano Maalumu wa CCM ambao jina
la mgombea huyo wa urais kupitia Chadema na Ukawa lilitajwa na makada wengi wa
chama hicho tawala.
Alisema hilo lilidhihirika hata
katika mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais, kutokana na Lowassa
kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa.
Alisema kitendo cha Waziri Mkuu
huyo wa zamani kuzua mjadala katika Mkutano Mkuu wa chama hicho tawala sambamba
na wimbi la makada wanaohama vyama vyao, si mambo yanayopaswa kuwa mjadala kwa
sababu uchaguzi ulishapita.
Huku akisema: “Sizungumzi haya kwa
ajili ya kujipendekeza, sihitaji ukuu wa wilaya,” Lusekelo aliwataka viongozi
kukataa kuendeleza uhasama wa kisiasa na chuki kwa maelezo kuwa mwaka huu uwe
maalumu kuzika tofauti hizo, kufanya kazi kulijenga Taifa na kuhubiri amani na
umoja.
Katika mkutano huo, Lusekelo
alipongeza kuimarika kwa vyama vya upinzani akaponda mvutano ulioibuka bungeni
akisema kukosa uzoefu kwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kulichangia huku akiunga
mkono kauli ya Rais kuzuia shughuli za siasa na kubainisha jinsi Rasimu ya
Katiba ya Tume ya Jaji Joseph Warioba, ilivyopendekeza kupunguzwa kwa madaraka
ya Rais.
Jumamosi iliyopita, katika Mkutano
Mkuu wa CCM mjini Dodoma, uliomalizika kwa Rais Magufuli kuchaguliwa kuwa
mwenyekiti, mzimu wa Lowassa ulitawala kutokana na kila aliyepewa nafasi ya
kuzungumza ama kumtaja kwa jina au kwa mafumbo.
Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda
wake, Jakaya Kikwete ndiye aliyeanza kuzungumzia hali ya mchakato wa chama
hicho kupata mgombea wake wa urais, kuwa ulikuwa mgumu na majaribu makubwa
na kwamba wazee walifanya kazi kunusuru hali hiyo.
Katika mchakato huo, CCM ilikata
jina la Lowassa katika hatua za awali, jambo lililosababisha kiongozi huyo
kuhama na kundi la wanaCCM na kujiunga na Chadema ambayo ilimteua kuwa mgombea
wake wa urais.
Hata hivyo, katika mkutano wake wa
jana, Lusekelo alisema katika mchakato wa chama hicho tawala kupata mgombea
wake wa urais kulikuwa na watu wenye majina makubwa, akiwamo Lowassa na
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.
“Niliwaambia CCM, Membe huwezi
kumpuuza, Lowassa naye huwezi kumpuuza maana wanataka madaraka na kwa vyovyote
lazima mtapata mtikisiko. Nikawaomba waahirishe suala la kupata Katiba Mpya
maana wasingelimaliza na muda ulikuwa mfupi,” alisema na kuongeza: “Kama
mwaka huu hautatumika kutibu majeraha yaliyotokea huko nyuma, tutaharibikiwa
sana.”
Alisema mchakato wowote wa uchaguzi
na kura ya maoni ndani ya vyama huacha mpasuko na watu hutumia dini na ukabila
kubaguana, hivyo lazima baada ya uchaguzi mambo hayo yamalizwe.
“Tunapaswa kukumbuka kuwa wote ni
Watanzania tusahau uchaguzi. Sasa ni wakati wa kuijenga nchi. Amani
inatengenezwa, na Mungu huwapa hekima maana kujenga ni kazi na kubomoa ni
rahisi, huu ni mwaka wa uponyaji na kurejesha Taifa pamoja,” alisema
Lusekelo.
Alisema kuanza kubagua watu kwa
sababu walitoka CCM kwenda Chadema au kutoka Chadema kwenda chama tawala si
jambo sahihi huku akitolea mfano mataifa yaliyovurugika kwa kuendekeza siasa za
chuki na uhasama.
Yaliyotokea bungeni
Akizungumza yaliyotokea bungeni na
kusababisha wabunge wa Ukawa kususia vikao vya Bunge vilivyoongozwa na Dk
Tulia, Lusekelo alisema Mtanzania anayejua historia ya nchi yake hawezi
kufumbia macho suala hilo.
“Binafsi nawalaumu waliotoka
(wabunge wa upinzani) na waliobaki (wabunge wa CCM). Kushindana si kuzuri.
Mbatia (James Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na wenzake
wanapaswa kujua kuwa naibu spika ni mchanga katika siasa waende naye taratibu
maana kapewa ubunge tu na kuwa naibu spika,” alisema.
Huku akiponda uamuzi wa Serikali
kufuta urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge alisema: “Nashangaa
wazee kama Salim (Ahmed Salim – Waziri Mkuu mstaafu), Pinda (Mizengo – Waziri
Mkuu mstaafu) na Warioba. Sijui walishindwa nini kukaa na wabunge hawa ili
kumaliza tofauti zao.”
Alisema si jambo jema kuongoza nchi
kwa mabavu na kusisitiza kuwa hata uhuru ulipatikana kwa mazungumzo.
Mchungaji huyo aliusifu utawala wa Rais Magufuli kuwa una kasi kubwa na kwamba licha ya wananchi kulia ukata, watacheka baada ya mwaka mmoja huku akiwananga wanaomponda Kikwete kuwa hawajui mazuri aliyoyafanya.
Mchungaji huyo aliusifu utawala wa Rais Magufuli kuwa una kasi kubwa na kwamba licha ya wananchi kulia ukata, watacheka baada ya mwaka mmoja huku akiwananga wanaomponda Kikwete kuwa hawajui mazuri aliyoyafanya.
Awapongeza wapinzani
Akizungumzia nguvu ya vyama vya upinzani, Lusekelo alisema ushindani wa kisiasa umekuwa mkubwa kutokana na kuimarika kwa upinzani: “Chadema ya sasa si ile ya miaka ya 1990. Wanaongoza miji mikubwa na ukiona chama kina wabunge 40 usikipuuze. Hata nguvu ya mfalme ni watu.”
Akizungumzia nguvu ya vyama vya upinzani, Lusekelo alisema ushindani wa kisiasa umekuwa mkubwa kutokana na kuimarika kwa upinzani: “Chadema ya sasa si ile ya miaka ya 1990. Wanaongoza miji mikubwa na ukiona chama kina wabunge 40 usikipuuze. Hata nguvu ya mfalme ni watu.”
Mikutano ya siasa
Kuhusu kauli ya Rais kusitisha shughuli za siasa hadi mwaka 2020, alisema jambo hilo linaweza kuonekana baya lakini lina unafuu mkubwa, kwamba Kenya wamelifanya na kufanikiwa kumaliza tofauti za kisiasa.
Kuhusu kauli ya Rais kusitisha shughuli za siasa hadi mwaka 2020, alisema jambo hilo linaweza kuonekana baya lakini lina unafuu mkubwa, kwamba Kenya wamelifanya na kufanikiwa kumaliza tofauti za kisiasa.
“Hivi watu 10,000 wakiandamana na
kusema Magufuli aliiba kura itakuwaje? Tuna askari wa kuwazuia! Nadhani
wanasiasa wafanye kazi ya utawala katika vyama vyao. Tutulie kwanza tutibu
majeraha. Hakuna jambo baya kama kuwaongoza watu wenye njaa maana hawana la
kupoteza,” alisema.
Hata hivyo, Lusekelo alisema Rasimu
ya Katiba ilipendekeza Rais kupunguziwa madaraka na huenda madaraka makubwa
aliyonayo Rais yakawa sababu ya nchi kuendelea kuwa na amani.
“Kenya kuzuia maandamano ni ngumu
sana lakini hapa kwetu hadi Zitto (Kabwe-Kiongozi wa ACT-Wazalendo) alizuiwa
kufanya mkutano wa ndani. Kwetu rais ana madaraka makubwa sana,” alisema
huku akiwataka polisi kutekeleza wajibu wao vyema, wakikumbuka kuwa nao ni
binadamu.

No comments:
Post a Comment