
MAJENGO ya madarasa tisa, ofisi za
walimu nne, maabara na vyoo katika shule ya sekondari Lindi, vimeteketea kwa
moto, unaodaiwa kutokana na hitilafu ya umeme.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi,
Renatha Mzinga aliwaambia waandishi wa habari kwamba moto huo ulianza saa 7
usiku wa kuamkia jana.
Alisema kikosi cha Zimamoto
kilifika eneo la tukio, lakini kutokana na tatizo la kiufundi, walishindwa
kufanya kazi ipasavyo.
Kwa mujibu wa kamanda, lililetwa
gari la polisi lenye maji ambayo hutumika wakati wa kutuliza ghasia maarufu
kama ‘washawasha’ likasaidia kazi ya kuzima moto, kabla ya kudhibitiwa
kikamilifu asubuhi ya jana. Hata hivyo alisema wakati jamii ikihangaika kuzima
moto huo, mmoja wa watu alikamatwa akidaiwa kuiba kompyuta mpakato.
Ingawa hakuna mtu aliyekufa,
kamanda alisema vifaa mbalimbali vilivyokuwamo madarasani, ofisi za walimu na
maabara, vimeteketea vyote.
Wananchi waliozungumzia ajali hiyo,
walilalamikia utendaji wa kikosi cha Zimamoto kwa kusema si mzuri.
Kwa mujibu wa mashuhuda, gari la
Zimamoto lilipofika, madarasa mawili ndiyo yaliyokuwa yameteketea lakini
kutokana na kushindwa kuzima moto, uliendelea kusambaa na kuteketeza madarasa
tisa, ofisi za walimu na vyoo.
Taarifa zilieleza kuwa jana, Naibu
Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, Selemani Jafo alikuwa njiani kuja
mkoani hapa kuangalia tukio hilo.




No comments:
Post a Comment