
Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwafikisha mahakamani
wanachama wake wanne linaowashikilia kwa siku 12 sasa.
Mtandao huo umedai kuwa watu saba
wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana
Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo.
Mratibu wa THRDC, Onesmo
Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa wazi
jambo lililo kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa makosa ya
jinai.
“Hadi sasa watetezi wanne
wamenyimwa dhamana wakati wengine wenye nafasi za kisiasa wamepewa. Hii si
sawa,” alisema Olengurumwa.
Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa
ni Samwel Nangiria, Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati
walioachiwa ni mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa
Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros, Joshua
Makko.
Alieleza kuwa watetezi hao
wamenyang’anywa vitendea kazi vyao pamoja na vifaa vya mawasiliano zikiwamo
simu za mkononi na kompyuta mpakato.
Wakili wa Kujitegemea wa kampuni ya
Law Guards Advocates, Jebra Kambole alisema hiyo ni kinyume na sheria
zinazosimamia haki za binadamu nchini.
“Kumshikilia mtu muda mrefu bila
dhamana pamoja na kunyimwa uwakilishi ni kinyume na Katiba ya nchi. Ni kinyume
na Azimio la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998,” alisema
Kambole baada ya kueleza kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa haki ya kuwatumia
mawakili.
Licha ya ombi hilo kwa Polisi, mwanachama
wa mtandao huo, Rose Sarwatt alimuomba Jaji Mkuu kuingilia kati suala hilo ili
kuhakikisha haki inatendekea.
Aliziomba asasi za kimataifa
kukemea na kuishauri Serikali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea
huko Loliondo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Charles Mkumbo alisema jeshi lake linasimamia na kutekeleza sheria za nchi na
halichagui wa kumkamata kama amefanya kosa la jinai.
“Lazima ukamatwe labda uwe na
kinga. Hata mimi, japo kazi yangu ni kukamata lakini nikifanya jinai nitakamwa
tu,” alisema na kubainisha kuwa taratibu zinaendelea
kuzingatiwa na zikimalizika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

No comments:
Post a Comment