
Diwani wa Kata ya Kiborlon
(Chadema) katika Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma ameonyesha ujasiri wa hali ya
juu alipopambana na majambazi waliokuwa na silaha za moto.
Alinusurika kuuawa baada ya
majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola kumfyatulia risasi sita alipokuwa
akiwafukuza ambazo hata hivyo, hazikumpata.
Tukio hilo ambalo lilionekana kama
sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya majambazi hao kuvamia duka la
jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na Menti Mbowe na kupora Sh10
milioni.
Katika tukio hilo lililotokea saa
tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hao walimjeruhi kichwani
mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame Safaris.
Hali ya majeruhi huyo inaendelea
vizuri. Akisimulia tukio hilo, diwani huyo alisema siku hiyo akiwa maeneo ya
Kiborlon, alipigiwa simu kuwa mfanyabiashara huyo amevamiwa na majambazi ndipo
alipoendesha gari lake hadi eneo la tukio.
“Nilipofika pale wale majambazi
watatu ndiyo walikuwa wanatoka kwenye duka. Nikampelekea gari yule aliyekuwa ameshika
bunduki. Kuona hivyo akafyatua risasi hewani,” alisema
Kagoma.
“Yule mwenye bunduki akaingia
uchochoroni kuelekea Barabara ya Stendi ya Kidia. Mwenzake aliyekuwa na bastola
naye akawasha risasi nyingine hewani kunitisha,” alisema.
Baada ya hali hiyo, diwani huyo
alilazimika kujificha kwenye gari na majambazi hao walidandia pikipiki na
kuanza kukimbia kuelekea Barabara ya Msaranga, naye akawafuata kuelekea
huko.
“Wakati huo tayari vijana wangu wa
bodaboda wakawa nao wamesikia hilo tukio tukaanza kusaidiana kuwafukuza lakini
mbele kidogo pale Msaranga wale majambazi wakasimamisha pikipiki yao umbali wa
mita 30 kutoka nilipokuwa na mmoja wao mwenye bunduki alifyatua risasi mbili na
mwenye bastola risasi mbili kuelekea uelekeo wangu.
“Nililazimika kujificha kwenye
kiti, wale majambazi wakajua wameniua. Wakapanda tena pikipiki ili watoroke.
Nikawasha tena gari huku vijana wangu nao wakinisaidia tukaanza kuwafukuza,” alisema.
Kagoma alisema majambazi hao
walipita maeneo ambayo gari haliwezi kupita wakaelekea eneo la Mabogini Moshi
Vijijini hadi lango la TPC na baadaye wakaelekea Rundugai wilayani Hai.
“Kuna eneo vijana wangu wanasema
kulikuwa na vumbi sana, ndipo walipowapoteza na majambazi wakatoroka kupitia
njia ya reli ili kukwepa polisi waliokuwa wakiwasubiri mbele,” alisema na
kuongeza:“Hatukuwa na silaha, lakini tulijitahidi kupambana nao kwa ujasiri.
Tatizo nafikiri tulikosea kidogo. Ilitakiwa wakati tukifukuzana nao tuwape
polisi uelekeo wa majambazi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro,
Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa Jeshi lake litatoa taarifa rasmi kwa
wanahabari leo kuhusiana na msako unaoendeshwa na jeshi hilo.
“Kuna mambo tumeyafanya tangu tukio
hilo litokee lakini kesho (leo) saa sita mchana tutatoa taarifa rasmi pamoja na
mafanikio tuliyofikia hadi sasa. Tunaendelea vizuri na upelelezi,” alisema.
Kamanda Mutafungwa, alitoa wito kwa
wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ikiwamo kuwafichua wahalifu na mbinu
wanazozitua akisema polisi wamejipanga kukabili wimbi jipya la ujambazi.

No comments:
Post a Comment