Mwalimu wa Shule ya Msingi
Geitasamo iliyopo Kata ya Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Raphael
Charles (22) amenusurika kufa kwa kucharangwa mapanga kwa tuhuma za kumpa
ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Ikorongo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Geitasamo,
Marwa Meng’anyi alisema mwalimu huyo amejeruhiwa kwa kucharangwa mapanga na
watu wanaodaiwa kuwa ni kaka wa mwanafunzi huyo baada ya kuchukizwa na kitendo
cha dada yao (jina linahifadhiwa) kukatishwa masomo kwa kupata ujauzito.
Akizungumzia tukio la kucharangwa
mapanga, Mwalimu Charles alisema mkasa huo ulimkumba akiwa njiani kwenda
nyumbani akiwa ameongozana na mwalimu mwenzake aliyemtaja kwa jina la Frank
Batholomeo.
“Tukiwa njiani ghafla
walijitokeza na kuanza kunihoji kwa nini nimempa mimba mdogo wao, kabla
sijajibu mmoja wao alichomoa panga na kuanza kunishambulia akilenga kunikata
shingo,” alidai Charles.
Alidai katika jitihada za kujinusuru ilimbidi kutimua mbio, lakini alianguka chini na vijana hao kufanikiwa kumfikia na kuendelea kumshambulia kwa mapanga.
Alidai katika jitihada za kujinusuru ilimbidi kutimua mbio, lakini alianguka chini na vijana hao kufanikiwa kumfikia na kuendelea kumshambulia kwa mapanga.
Mwalimu huyo aliyefungua kesi
kuhusu shambulio hilo na kupewa namba ya jalada Mug/RB/2886/2016 la kujeruhi,
alidai alinusurika kuuawa baada ya mmoja wa mafundi pikipiki waliokuwa eneo
jirani kujitokeza kumsaidia.
Tukio la kushambuliwa kwa mwalimu huyo limekuja huku madai dhidi yake kumpachika mimba mwanafunzi huyo yakiwa yamefikishwa mahakamani kwa shauri namba 82/2016 tangu Mei 13.
Tukio la kushambuliwa kwa mwalimu huyo limekuja huku madai dhidi yake kumpachika mimba mwanafunzi huyo yakiwa yamefikishwa mahakamani kwa shauri namba 82/2016 tangu Mei 13.
Akizungumzia kitendo chake na
wanawe kumshambulia kwa mapanga mwalimu huyo, baba wa binti aliyepachikwa
mimba, Chacha Masiko alidai familia imechukizwa na kesi dhidi ya mwalimu huyo
kuahirishwa mara kwa mara bila wao kuelezwa sababu za msingi, huku mshtakiwa
huyo akiwatambia mtaani kuwa hatafungwa.
Mwalimu aliyeshuhudia mwezake
akicharangwa mapanga, Batholomeo alilaani kitendo cha wanafamilia hao
kujichukulia sheria mkononi na kuomba mamlaka husika kuchukua hatua kukomesha
vitendo hivyo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
Kaimu Ofisa Elimu wa wilaya hiyo,
Hawamu Tambwe alisema ameunda timu itakayoshirikiana na uongozi wa kijiji
kuelimisha wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria katika kushughulikia
changamoto na matatizo yanayojitokeza kwenye jamii badala ya kuchukua sheria
mkononi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara,
Ramadhani Ngh’azi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kutokana na simu yake
kuita bila kupokewa, lakini mmoja wa maofisa wa polisi wilayani hapa
aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema jeshi hilo linawasaka ndugu
hao ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

No comments:
Post a Comment