Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
inaendelea na maandalizi ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa kuboresha daftari
la wapiga kura ili kuweka taarifa za walengwa wakiwemo watakaopiga kura baada
ya kufikisha umri wa kupiga kura.
Aidha, itawahusu walioshindwa
kupiga kura katika chaguzi zilizopita kutokana na sababu mbalimbali. Hayo
yalisemwa jana mjini Kibaha na Ofisa Uchaguzi wa Tume hiyo, Adam Nyando wakati
akikabidhi taarifa za Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa mkoa wa Pwani.
Alisema, baada ya kumalizika kwa
uchaguzi wa mwaka 2015, wameanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao na si kwamba
kwa sasa Tume imelala.
“Watu wanafikiri uchaguzi
ukishaisha ndio kazi imekwisha kumalizika kwa uchaguzi mmoja ni maandalizi ya
uchaguzi ujao kwani kwa sasa tunaendelea na uboreshaji wa daftari la wapigakura
pamoja na kura za maoni,” alisema Nyando.
Alisema uchaguzi uliopita ulikwenda
vizuri na hakukuwa na matatizo makubwa licha ya matumizi ya mfumo mpya wa BVR,
lakini matokeo yake umekuwa mfumo mzuri na umepata mafanikio makubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist
Ndikilo, akizungumza alitumia fursa hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kufanya
uchaguzi mzuri usiokuwa na vurugu wala uvunjifu wa amani.
Ndikilo alisema nchi nyingine
kipindi cha uchaguzi ni kipindi kibaya cha uvunjifu wa amani, ikiwa ni pamoja
na umwagikaji mkubwa wa damu, hasa kwa pande zisizokubaliana matokeo.
“Uchaguzi ulienda vizuri licha ya
changamoto zilizojitokeza za hapa na pale lakini watu walivumiliana na
kukubaliana na matokeo kilichobaki sasa ni kufanya kazi ili kuwaletea maendeleo
wananchi, kikubwa ni tume kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza ikiwa ni
pamoja na usafiri na ucheleweshwaji wa matokeo kwa baadhi ya sehemu,” alisema
Ndikilo.
Akikabidhi taarifa hizo kwa Mkuu wa
Mkoa wa Pwani, Ofisa Uchaguzi wa mkoa, Shangwe Twamala alisema mkoa huo umepata
nakala 47 ambazo zitasambazwa kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi.
Alisema taarifa hizo zitasambazwa
kwenye ofisi za mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za
miji na wilaya na taasisi za elimu ya juu.

No comments:
Post a Comment