Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi na Mbunge wa jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) amezungumzia
jinsi alivyopokea kutumbuliwa kwake na Rais John Magufuli ambaye anaamika kuwa
rafiki yake akisema hawezi kuhoji uamuzi huo.
Kitwanga aliwaaambia waandishi wa
habari nyumbani kwake Misungwi kuwa ingawa hawezi kuhoji uamuzi huo, kuna kundi
kubwa la wauza madawa ya kulevya ndio waliolikuza tukio hilo kwa lengo la
kumchongea hadi kuondolewa kwenye nafasi hiyo.
“Anayofanya Dk. Magufuli nampongeza
sana kwani ni mtu ambaye namfahamu. Ni mwadilifu, msikivu, namshukuru kwa
kuniamini kufanya kazi naye katika Serikali yake hivyo siwezi kuhoji alichoamua
kwa sababau aliyetoa ndiye aliyeondoa,” alisema Kitwanga.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo
wa Misungwi alikana kuhusika kwa namna yoyote katika sakata la kampuni ya
Lugumi Enterprises Ltd iliyopewa zabuni ya kufunga mashine za kutambua alama za
vidole kwenye vituo vya polisi nchini, na kudaiwa kulipwa kiasi kikubwa cha
fedha wakati kazi haikufanyika kama ilivyotarajiwa. Sakata hilo bado lipo
katika uchunguzi japo dalili za kujadiliwa bungeni zinaonekana kufifia.
“Rais wa Kwanza wa Tanzania hayati
Mwalimu Julius Nyerere, kuna wakati alituhumiwa akidaiwa kuwa na mpango wa
kumpindua Rais wa Kenya baada ya kuzuru nchini humo. Alipoulizwa na waandishi
wa habari alijibu, ‘hivi mtu akikwambia mimi ni mume wa mama yako utakubali?’,
sasa hilo ndilo jibu langu kwa Watanzania ili wasiniulize tena,” alisema Kitwanga.
Akizugumzia umiliki wa kampuni ya
Infosys, alisema kuwa yeye ni mwanzilishi tu wa kampuni hiyo na hivi sasa
inamilikiwa na mwanae baada ya kumuuzia asilimia 33 ya hisa zake na kwamba
taarifa ya mauzo hayo ziko wazi.

No comments:
Post a Comment