Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia
Akson amesema hoja ya wabunge wa Ukawa kutaka aenguliwe kwenye wadhifa huo
inafanyiwa kazi na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo iwapo
itaridhia, itarejeshwa bungeni kupigiwa kura ambazo hata hivyo, hazitatosha kwa
uchache wao.
Dk Tulia alisema hayo jana wakati
akihojiwa na Tido Mhando katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Azam TV.
“Hoja ikishakuja bungeni hapo sasa
huwa ni kampeni na baadaye kupigiwa kura. Kwa kuwa waliopeleka hoja ni wabunge
wa upinzani, hivyo wanatakiwa kufikisha idadi fulani ambayo kiuhalisia wao kwa
sasa hawana,” alisema.
Kwa karibu mwezi mzima kwenye Bunge
la Bajeti, wabunge wa Ukawa walimsusia Dk Tulia na walikuwa wakitoka bungeni
kila alipoingia, tayari wameanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani kwa madai
kuwa hawatendei haki na anaminya demokrasia ndani ya Bunge.
Dk Tulia alisema Katiba inatambua
kwamba kiongozi aliyechaguliwa anaweza kuondolewa madarakani na wale
waliomchagua, hivyo wabunge wa upinzani wametumia haki yao ya msingi na
kinachosubiriwa ni hoja yao kufanyiwa kazi.
“Kanuni imeweka wazi na msingi ule
umejengwa kwenye Katiba kwa sababu inatambua wale waliomchagua kiongozi
wasiporidhika naye wanaweza kumuondoa madarakani. Nafarijika kuona wanachukua
hatua, hivyo mimi sina malumbano nao,” alisema.
Hakuna maridhiano
Dk Tulia alisema hakuna maridhiano
yanayotakiwa baina yake na wabunge wa Ukawa kwa kuwa hana malumbano nao, bali
kanuni na taratibu zinafuatwa kufanikisha hoja yao ya kumuondoa madarakani.
Naibu Spika huyo alisema maridhiano
huwapo baina ya watu wanaolumbana na kwamba, baina yao hakutakuwa na suala
hilo.

No comments:
Post a Comment