
Licha ya lori lililokosa breki
katika Mlima Iwambi nje kidogo ya Jiji la Mbeya, kuyakwepa magari manne,
limeyagonga mengine manne na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi
22.
Ajali hiyo ilitokea juzi usiku
katika mji mdogo wa Mbalizi, Barabara Kuu ya Mbeya - Tunduma, ambako lori hilo
liligonga basi aina ya Toyota Coaster na magari madogo matatu.
Katika tukio hilo, watu
watatu walifariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali Teule ya Ifisi na
hadi tunakwenda mitamboni walikuwa hawajatambuliwa, huku mwingine
aliyetambuliwa kwa jina Philip Cheyo (39) akifariki jana asubuhi katika
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Ifisi,
Elimate Sanga alisema walipokea miili ya watu watatu na majeruhi 22 wakiwamo
sita waliohamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kutokana na hali zao kuwa
mbaya. Sanga alisema hadi jana asubuhi, ali- kuwa na wagonjwa 12
waliolazwa.
Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali
ya Rufaa, Lucy Elias alisema Cheyo ambaye alikuwa mmoja wa majeruhi sita,
alifariki jana asubuhi akiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu
(ICU).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,
Dhahiri Kidavashari alisema wanachunguza chanzo cha ajali hiyo ingawa taarifa
za awali zinaonyesha kuwa lori lilifeli breki wakati likiteremka mlima
huo.
Akisimulia tukio hilo, kondakta wa
lori hilo, Wilberd Joseph akiwa wodi ya nne ya Ifisi alisema lilianza kuongeza
mwendo wakati wakianza kuteremka mlima huo na ndipo dereva akalalamika halina
breki.
“Nilisikia dereva ananiambia,
tuombe Mungu, breki zimegoma kabisa, ndipo lori likazidi kuchanganya na dereva
alijitahidi kuyakwepa magari zaidi ya manne hivi, lakini tulipoingia mjini
kabisa (Mbalizi), kulikuwa na (basi dogo) Hiace ikitokea upande wa kushoto
kuingia barabara kuu, alipolikwepa tela likagonga basi jingine aina ya Coaster
lililokuwa limesimama upande wa kulia,” alisema kondakta huyo.
Alisema baada ya kugonga basi hilo
lililokuwa likitokea Tunduma kwenda Mbeya, pia liligonga magari mengine
yaliyokuwa nyuma ya Coaster hiyo.
Mmoja wa majeruhi wa basi hilo,
Isack Mwaipaja aliyelazwa katika Hospitali ya Ifisi, alisema walipofika Mbalizi
dereva wao hakutaka kuingia stendi na aliamua kuteremsha abiria pembeni mwa
barabara kuu ndipo ghafla wakasikia kishindo.
“Bila kujua kinachoendelea
nikajiona nimelowa usoni, kupangusa hivi nikaona damu inavunja usoni, kumbe ni
lori lilikuwa limetugonga ubavuni na wale waliokuwa nyuma ya basi ndiyo
walioumia sana kwani tela lote liliishia huko,” alisema.

No comments:
Post a Comment