RAIS John Magufuli amesema
wakurugenzi watendaji (DED) wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji
aliowateua hivi karibuni, hakuwachagua kwa kubahatisha wala hakuchagua vilaza.
Pamoja na hayo, Magufuli ametoboa siri ya kuihamishia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) chini ya Ofisi ya Rais kuwa ni baada ya kubaini miaka ya nyuma nafasi za ukurugenzi zilikuwa zinatolewa kwa ushawishi na rushwa.
Rais alisema hayo Ikulu Dar es
Salaam jana katika hafla fupi ya viongozi hao wapya ya kula kiapo cha Uadilifu
wa Uongozi wa Umma kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na
kupatiwa semina ya maadili ya viongozi wa umma.
Alisema tangu awateue wakurugenzi
hao kumekuwa na maneno ya chinichini na mitandao ya kijamii, ikidai kuwa wengi
wao hawana sifa na kufikia hatua ya kumtaja Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Wilaya
ya Itigi mkoani Singida, Pius Shija Luhende kuwa ni mhudumu wa hoteli iliyopo
Sinza jijini Dar es Salaam.
Ma-DED wana sifa za kutosha
“Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano
ni kuwatumikia wananchi na kutimiza ahadi pamoja na Ilani ya CCM ya mwaka 2015
kwa kipindi cha miaka mitano. Tayari hadi sasa miezi minane imeshapotea, nataka
utekelezaji wa ahadi hizi uende kwa kasi ya ajabu…
“…Sasa kwa kasi hii ninayoitaka siwezi kubahatisha katika uteuzi wa viongozi watakaofanikisha azma hii. Hawa wakurugenzi niliowachagua asilimia 80 wana Shahada ya Uzamili na wengine wana Shahada na uzoefu wa kutosha,” alisisitiza Rais Magufuli.
“…Sasa kwa kasi hii ninayoitaka siwezi kubahatisha katika uteuzi wa viongozi watakaofanikisha azma hii. Hawa wakurugenzi niliowachagua asilimia 80 wana Shahada ya Uzamili na wengine wana Shahada na uzoefu wa kutosha,” alisisitiza Rais Magufuli.
Kuhusu uteuzi wa Shija, alisema
anafahamu kuwa mkurugenzi huyo ana sifa za kutosha kuitumikia nafasi hiyo kwa
kuwa ana Shahada ya Uzamili na Stashahada na alikuwa ni mkaguzi wa shule.
“Unajua baada ya hili la mitandao
ya kijamii nimejifunza mengi, ukiona adui anakushangilia ukifanya jambo, rudi
nyuma ujiulize umekosea wapi lakini ukiona adui yako anakushambulia basi ujue
umemtwanga,”alisema Rais Magufuli.
Alisema anafahamu kuwa nafasi ya
ukurugenzi wa halmashauri ni muhimu katika kujenga uchumi hasa wa chini ndio
maana katika kuwateua viongozi hao, ametumia takribani miezi minne kuwachuja na
kuwachambua ili kupata viongozi wenye sifa na vigezo stahili.
Hongo kupata u-DED
Alisema zamani wakurugenzi wengi
walikuwa wakipata nafasi hiyo kwa kufanya ushawishi kwa kushirikiana na maofisa
wa Tamisemi na kuwahonga fedha.
“Pale Tamisemi kulikuwa na timu
imejipanga kufanikisha hili. Nimeshaagiza waziri ahakikishe watu wote
waliohusika kwa hili wanaondolewa ndio maana niliamua wizara hii iwe chini
yangu kwa makusudi,” alifafanua.
Akizungumzia uwajibikaji wa
wakurugenzi hao, alisema fedha nyingi za serikali hupelekwa kwenye halmashauri,
eneo ambalo limekuwa na sifa mbaya ya fedha hizo kutumika hovyo bila kuzingatia
weledi na maadili.
Alisema ndio maana katika uteuzi wa
wakurugenzi hao kati ya wakurugenzi 185 waliokuwapo, wa zamani walioendelea ni
60 pekee na 120 ‘wametemwa’, hali inayodhihirisha kuwa waliobaki ni watendaji
wazuri ambapo yeye aliwaita ‘majembe’.
Alisema kila mkurugenzi
aliyechaguliwa, atambue kuwa sifa zake zilichambuliwa na Rais mwenyewe. “Ndio
maana mimi sitembei, nilikuwa nalala saa sita hadi saa nane usiku, nawafahamu
wote kwa sifa hadi majina, ninaamini hawataniangusha,” alisema.
Aliwataka kuhakikisha wanazisimamia
vyema fedha za serikali zinazowasilishwa katika halmashauri na kuepuka
kuburuzwa, kujipendekeza, kukejeliwa au kutumika vibaya kwa kuingia mikataba na
kampuni feki zisizoweza kutekeleza vyema wajibu wake.
Fedha za Mfuko wa Barabara
Magufuli alisema anazo taarifa za
baadhi ya wakurugenzi, walikuwa wakishirikiana na mameya, madiwani na wenyeviti
wa halmashauri kwa kupitisha na kuingia mikataba na kampuni zilizo na uwezo
chini ya viwango katika kutekeleza miradi ya barabara; na matokeo yake miradi
mingi haikuwa na mafanikio.
“Nawaambieni mkisimamia maadili
hakuna atakayewafukuza kazi. Msijipendekeze kwa mtu kwa sababu hakuna
aliyepenyeza majina yenu kwangu hadi mkachaguliwa. Kuna mmoja jina lake
lilipenyezwa nikalitupilia mbali,” alisema.
Fedha za elimu bure
Aliwataka kuwa makini na kusimamia
vyema Sh bilioni 18.77 zinazotolewa na serikali kila mwezi kwa ajili ya elimu
bure katika shule za msingi na sekondari kwa kuhakikisha zinatumika vyema kwa
lengo lililokusudiwa.
Alisema wapo wakurugenzi waliokuwa
wakizitumia vibaya fedha hizo kwa madai kuwa ni nyingi, huku kukiwa na taarifa
za baadhi ya walimu wakuu katika kufanya udanganyifu kwa kuandika orodha ya
uongo ya wanafunzi na kuongeza idadi ili wapate mgawo mkubwa wa fedha hizo.
Matumizi ya EFDs serikalini Pamoja
na hayo, Rais Magufuli aliziagiza wizara zote nchini chini ya makatibu wake
wakuu na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji na taasisi zote za
serikali, kuhakikisha wanaanza mara moja kukusanya mapato yake kwa kutumia
mashine za kielektroniki (EFDs).
“Haiwezekani mfanyabiashara
alazimishwe kutumia mashine hizi wakati sisi serikalini tunakusanya mapato yetu
bila kutumia mashine za EFDs. Ninawataka nyie wakurugenzi mliopo hapa mkifika
katika maeneo yenu mhakikishe halmashauri zenu zinakusanya mapato yake kwa
kutumia EFDs,” alisisitiza.
Aidha aliwaagiza wakurugenzi hao
kuhakikisha wanashiriki katika kutimiza ndoto ya Tanzania kuwa taifa lenye
kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda kwa kila mmoja kuhakikisha katika
eneo lake kunaanzishwa viwanda vidogo.
Kodi ndogo ndogo
Akizungumzia kero na changamoto
zinazowakabili wananchi, Dk Magufuli aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha
kipaumbele chao kikubwa kinakuwa ni kuondoa kero za wananchi hasa wale wenye
maisha ya chini.
Alisema watanzania wamekuwa
wakiteseka kwa muda mrefu na kuhangaishwa na kodi za ajabu hali iliyochangia
kurudisha maisha yao nyuma.
“Unakuta mtu analima mpunga wake,
akivuna na kuubeba kuupeleka nyumbani kwa matumizi anadaiwa kodi, mbona wakati
analima hamkudai kodi? “Nawaomba mhakikishe kodi za aina hii mnazizuia kwani
Serikali hii wakati ikiomba kura ya kuingia madarakani, haikuahidi kutengeneza
kero kwa wananchi bali kuziondoa kero hizo,” alisema.
Kutumbua majipu
Aliwaagiza wakurugenzi hao
watakapofika kwenye vituo vyao vya kazi, kuhakikisha wanachukulia hatua na
kuwaondoa mara moja watendaji walio kwenye mamlaka yao wasiowajibika na wale
wanaofanya kazi kwa kujifanya miungu watu.
“Nina taarifa wapo watendaji kata
ambao wanajifanya miungu watu, kazi yao kubwa ni kuichonganisha Serikali na
wananchi, tumieni madaraka yenu kuwaondoa ila msimuonee mtu. Nataka mkawe
mitume kwa niaba ya Serikali,” alisema.
Magufuli alisema amewateua viongozi
hao kwa kuwaamini na hatarajii itafika siku atajutia uteuzi wake na kubaini
kuwa aliwateua kimakosa.
Makamu wa Rais
Kwa upande wake, Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao
kwa kuwa kuhudumia na kusimamia watumishi wa umma na wananchi; na si kuwa
watawala.
“Kila mtu ajiulize kwa nini
Tanzania kwenye watu takribani milioni 50, lakini ameteuliwa yeye. Someni alama
za nyakati na muwatumikie vyema wananchi. Someni pia mazingira ya kazi,
simamieni utendaji wenu kwa misingi ya sheria na katiba,” alisema
Samia.
Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
alisema nafasi ya ukurugenzi katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na
majiji ni sawa na injini ya uwajibikaji, hivyo wanaoshika nafasi hizo
wanatakiwa kuwa wachapakazi, waadilifu na wenye kujituma ili serikali na taifa
kwa ujumla lifikie malengo yake.
“Nawataka mkifika muanze kwanza
kuwafahamu vyema washirika wenu kama vile mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, kamati
ya ulinzi na usalama, sekretarieti ya mkoa, wakuu wa idara na watumishi.
Zijueni vyema ofisi zenu tambueni maeneo yenu ya kazi,” alisema Majaliwa.
Aidha, alisema halmashauri pamoja
na kuendeshwa kwa fedha za serikali pia zina vyanzo vyake vya ndani vya mapato
na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kusimamia vyema vyanzo
hivyo na ukusanyaji wa mapato yake.
Aliwataka kuwa mstari wa mbele
kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo ya Rais likiwemo agizo lake la hivi
karibuni la kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari ana
dawati.
Ma-DC
Pamoja na wakurugenzi hao kuapa kiapo cha uadilifu, pia wakuu wa wilaya watatu ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu, Agnes Hokororo (Manyoni - Singida) na Miraji Mtaturu (Ikungi – Singida) walikula kiapo hicho.
Pamoja na wakurugenzi hao kuapa kiapo cha uadilifu, pia wakuu wa wilaya watatu ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu, Agnes Hokororo (Manyoni - Singida) na Miraji Mtaturu (Ikungi – Singida) walikula kiapo hicho.
Ma-DC hao hawakula kiapo cha
uadilifu na wenzao hivi karibuni baada ya kubainika makosa katika uteuzi wa wateule
wa awali wa nafasi za wilaya hizo. Hokororo alichukua nafasi ya aliyeteuliwa
kuwa mkuu wa wilaya hiyo awali, Fatma Toufiq kutenguliwa kwa kuwa tayari ana
wadhifa wa ubunge Viti Maalumu.
Babu na Mtaturu walichukua nafasi
hizo baada ya wateule wa awali ambao ni Fikiri Avias Said na Emile
Ntakamulenga, kutenguliwa uteuzi wao baada ya kuteuliwa kimakosa.
Kwa upande wake, Kamishna wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda aliwataka
viongozi hao kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ikiwemo
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha, aliwataka kuhakikisha
wanatunza maadili yao kama viongozi wa umma na kutambua kuwa wao na viongozi wa
umma kwa saa 24 usiku na mchana hivyo wajiepushe na masuala yatakayowavunjia
heshima na kuwaaibisha mbele ya jamii.
“Lakini pia nawahimiza mkumbuke
kuwa nyie mtakuwa na siri nyingi za serikali haitopendeza kumkuta mbunge ana
nyaraka zilizoandikwa siri za serikali kutoka eneo lako. Moja kwa moja
utajibu,” alisema.
Jaji Kaganda alisema amebaini kuwa
wateule wengi wa nafasi hizo za wakurugenzi ni vijana na kuwahimiza kuhakikisha
hawaleweshwi na madaraka hayo na kujiingiza kwenye matendo ya anasa na
kujivunjia heshima.

No comments:
Post a Comment